Wataalam wasema Ubaguzi wa rangi, maslahi binafsi ya kisiasa yanachochea vurugu za ufyatulianaji risasi nchini Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 09, 2022

Bendera ya Marekani ikipepea nusu mlingoti juu ya Ikulu ya Marekani, White House huko Washington, D.C., Marekani, Mei 24, 2022. (Picha na Ting Shen/Xinhua)

CAIRO - Katika wiki za hivi karibuni Marekani imetikiswa na mfululizo wa mashambulizi ya kufyatuliana risasi na kuua wakazi 10 wamarekani wenye asili ya Afrika katika duka kubwa mjini New York, watoto 19 na walimu wawili huko Texas, na watu wanne katika kituo cha afya huko Oklahoma.

Wataalamu kutoka eneo la Mashariki ya Kati wamesema, vurugu za ufyatulianaji risasi ambazo hazijadhibitiwa ni matokeo ya dhuluma zenye misingi ya ubaguzi wa rangi na maslahi binafsi ya vyama vya siasa na makundi yenye nguvu ya uzengezi yanayounga mkono bunduki nchini humo.

Dhuluma za ubaguzi wa rangi

"Wengi wa waathirika wa ghasia si watu weupe," amesema Ezzat Saad, Mkurugenzi wa Baraza la Masuala ya Kigeni la Misri, akirejelea mauaji ya hivi karibuni ya watu wengi nchini Marekani.

Amesema kukithiri kwa vurugu za ufyatulianaji risasi nchini Marekani ni matokeo ya ubaguzi wa rangi unaoendekezwa na watu wenye itikadi kali za mrengo wa kulia, ambao wanaamini kuwa "watu weupe ni bora kuliko rangi nyingine."

"Tatizo ni kwamba mawazo hayo yenye msimamo mkali yameingia kwenye vyama vya siasa na kuanza kutafuta njia ndani ya taasisi za maamuzi," Saad ameongeza.

Maoni ya Saad yanauungwa mkono na Suzan Ismail, mwanasheria wa Lebanon, ambaye amesema kwamba ingawa sheria za Marekani zinapiga marufuku ubaguzi wa rangi, vitendo hivyo bado vimeenea sana nchini humo.

Vyama vyenye maslahi binafsi na wazengezi wa bunduki

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, vurugu za kutumia bunduki nchini Marekani zimeongezeka licha ya wito wa kuweka udhibiti mkali wa bunduki.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi majuzi iliyotolewa na Ofisi ya Upelelezi ya Serikali Kuu ya Marekani, kulikuwa na "matukio 61 ya ufyatuaji risasi" Mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 52.5 kutoka Mwaka 2020 na kwa asilimia 96.8 kutoka Mwaka 2017.

Wanafunzi waliovalia fulana za kuzuia risasi wakifanya mkutano karibu na bwawa la Capitol Reflecting huko Washington, D.C., Marekani, Juni. 6, 2022. (Picha na Aaron Schwartz/Xinhua)

Mtaalam Ismail amehusisha ongezeko la vurugu za kutumia bunduki nchini Marekani na kutokuwepo kwa sheria zinazofaa za kuzuia watu wa kawaida kupata bunduki.

“Upatikanaji wa silaha kwa urahisi, na bei nafuu ya silaha huwawezesha hata wanafunzi kuzinunua na kuzitumia sehemu zisizo mwafaka.”

Shirikisho la Taifa la Bunduki (NRA), shirika kubwa zaidi la wamiliki wa bunduki nchini Marekani, ambalo linadai kuwa na wanachama takriban milioni 5, limekuwa likifanya uzengezi mkubwa dhidi ya kupitisha sheria zozote za kudhibiti bunduki katika Bunge la Marekani kwa kutumia mamilioni ya dola kila mwaka katika uzengezi wa kisiasa.

Mbaya zaidi, vyama vya siasa vya Republican na Democrats, ambavyo huhitaji fedha kwa ajili ya kampeni za uchaguzi ili kupata kura zinazohitajika, vinahofia kuwakera wafuasi wa bunduki wakiongozwa na NRA. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha