Zanzibar yaapa kutokomeza utumikishwaji wa watoto wakati ikiadhimisha siku ya kupinga ajira kwa watoto duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 13, 2022

DAR ES SALAAM – Serikali ya Zanzibar nchini Tanzania jana Jumapili kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira kwa Watoto iliapa kuwa itatokomeza utumikishwaji wa watoto.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema tangu Mwaka 2005 mamlaka za serikali visiwani humo zimekuwa zikichukua hatua zinazolenga kukabiliana na utumikishwaji wa watoto.

"Serikali imetunga sheria zinazotoa ulinzi wa watoto dhidi ya ajira kwa watoto," Soraga amesema kwenye mkutano na wanahabari.

Amesema kuna watoto wapatao 25,803 wenye umri kati ya miaka mitano na 17 wanaotumikishwa visiwani Zanzibar.

“Takriban watoto 2,256 wakiwemo wasichana 840 wameokolewa kutoka kwenye utumikishwaji wa watoto katika maeneo tofauti ya visiwa pacha vya Unguja na Pemba”, amesema Soraga.

Shirika la Kazi Duniani lilianza kuadhimisha Siku ya Dunia ya kupinga ajira kwa watoto Mwaka 2002 ili kuangazia masaibu ya watoto ambao ni waathiriwa wa ajira za watoto.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha