

Lugha Nyingine
Kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira chakaribia Marekani huku Benki Kuu ikipambana na mfumuko wa bei: WSJ
Wafanyakazi wakiwa kwenye soko la chakula huko Washington, D.C., Marekani, Mei 6, 2022. (Picha na Ting Shen/Xinhua)
NEW YORK - Makala iliyochapishwa Jumatatu wiki hii na Jarida la The Wall Street inasema, maofisa wa Benki Kuu ya Marekani wanaanza kuashiria kwamba jitihada zao za kukabiliana na mfumuko wa bei kwa kuinua viwango vya riba huenda zikasababisha ukosefu mkubwa wa ajira.
Imesema kwamba, hii inaashiria mabadiliko kutoka mwaka jana, walipotafuta urejeshaji wa haraka wa soko la ajira.
Makala hiyo inatarajia kuwa Benki Kuu inaweza kuzingatia kuongeza viwango vya riba kwa alama za msingi zinazofikia 75 wiki hii kwani mfumuko wa bei unabaki kuwa juu na watunga sera wanakadiria kutokea kwa viwango vya juu vya ukosefu wa ajira katika miaka miwili ijayo kuliko vile walivyotarajia mapema mwaka huu.
Mwenyekiti wa Benki Kuu ya Marekani, Jerome Powell na maafisa wengine walipendekeza mapema mwaka huu kwamba wanaweza kupunguza uhitaji wa wafanyakazi – ambacho ni chanzo cha shinikizo la mfumuko wa bei -- kimsingi kwa kuwahimiza waajiri kupunguza nafasi za kazi, badala ya kuwaachisha kazi wafanyakazi na kuongeza ukosefu wa ajira.
Makala hiyo imeeleza kwamba, lakini katika maoni yao ya hivi majuzi, maafisa wa Benki Kuu wameweka mkakati ambao unafanya ukosefu wa ajira uongezeke mwaka huu, ingawa siyo kwa kasi.
“Baadhi ya wanauchumi wamekuwa na mashaka kwamba Benki Kuu inaweza kupunguza nafasi za kazi bila kuinuliwa juu kwa kiwango cha ukosefu wa ajira”, inasema makala hiyo.
Pia inaonya kwamba "tunapaswa kujitayarisha kwa makadirio yanayokusudiwa kuwasilisha maamuzi ya Benki Kuu ya kupunguza mfumuko wa bei kwa kulenga kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira," akimnukuu Tim Duy, mwanauchumi mkuu wa Marekani katika Taasisi ya Utafiti ya SGH Macro Advisors.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma