Rais Xi Jinping wa China azungumza na Putin kwa njia ya simu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 16, 2022

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping Jumatano alasiri alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin.

Katika mazungumzo yao, Xi alibainisha kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, uhusiano kati ya nchi hizo mbili umedumisha kasi nzuri ya maendeleo katika kukabiliana na misukosuko na mabadiliko ya kimataifa.

“Ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizi mbili umepata maendeleo thabiti”, Xi alisema, huku akiongeza kuwa daraja la barabara kuu ya kutoka Heihe, China hadi Blagoveshchensk, Russia limefunguliwa rasmi kwa matumizi, na kutengeneza njia mpya inayounganisha nchi hizo mbili.

Xi alisema, upande wa China uko tayari kushirikiana na upande wa Russia katika kusukuma maendeleo thabiti na ya muda mrefu ya ushirikiano wa kivitendo baina ya nchi hizo mbili.

Xi amesema, China inapenda kushirikiana na Russia ili kuendelea kusaidiana katika maslahi yao ya msingi kuhusu mamlaka na usalama wa taifa, pamoja na masuala yao makuu, kuimarisha uratibu wao wa kimkakati, na kuimarisha mawasiliano na uratibu katika mashirika muhimu ya kimataifa na kikanda kama vile Umoja wa Mataifa, utaratibu wa BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.

“China pia inapenda kushirikiana na Russia ili kuhimiza mshikamano na ushirikiano kati ya nchi zenye masoko yanayoibuka na zile zinazoendelea, na kusukuma maendeleo ya utaratibu na usimamizi wa dunia nzima ili kuelekea kwenye mwelekeo wa haki na busara zaidi.

Kwa upande wake, Putin alisema upande wa Russia unaipongeza kwa dhati China kwa mafanikio yake makubwa ya kimaendeleo chini ya uongozi thabiti wa Xi.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, ushirikiano wa kivitendo kati ya Russia na China umekuwa ukiendelezwa kwa kasi, na kuongeza kuwa Russia inaunga mkono Pendekezo la Usalama wa Dunia Nzima lililopendekezwa na upande wa China, na inapinga nguvu yoyote ya kuingilia masuala ya ndani ya China kwa kutumia kile kinachoitwa masuala kuhusu Xinjiang, Hong Kong na Taiwan, miongoni mwa mengine, kama kisingizio.

Alibainisha kuwa Russia iko tayari kuimarisha uratibu wa pande nyingi na China ili kufanya juhudi za kiujenzi katika kuhimiza uhusiano wa pande nyingi za Dunia, na kuweka utaratibu wa kimataifa wenye haki na unaokubalika zaidi.

Wakuu hao wa nchi pia walibadilishana mawazo kuhusu suala la Ukraine. Katika hili Xi alisisitiza kuwa, China daima imekuwa ikitathmini hali kwa kujiamulia na kwa msingi wa muktadha wa kihistoria na umuhimu wa suala husika, na kufanya juhudi za kuhimiza amani ya Dunia na utulivu wa utaratibu wa uchumi wa Dunia.

Pande zote zinapaswa kushinikiza kutatuliwa mgogoro wa Ukraine kwa njia inayofaa na kwa njia ya kuwajibika, Xi alisema, akiongeza kuwa China kwa ajili hiyo itaendelea kutekeleza jukumu lake linalostahili.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha