

Lugha Nyingine
Maandamano ya amani yafanyika Kaskazini Mashariki mwa DRC dhidi ya waasi wa M23
GOMA, DRC - Maelfu ya watu wameandamana Jumatano wiki hii katika Mji wa Goma, Mji Mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kupinga mashambulizi ya hivi karibuni ya waasi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23) ambao walichukua udhibiti wa mji wa mpakani wa Bunagana siku chache zilizopita.
Siku ya Jumatano, jumuiya za kiraia na mavuguvugu ya vijana yaliandaa maandamano ya amani kupinga kuanguka kwa Mji wa Bunagana, ambao ni kituo muhimu kwa biashara za mipakani kati ya DRC na Uganda. Mji wa Bunagana pia umewahi kutekwa na waasi wa M23 Mwaka 2012.
Likiwa ni kundi linalotokana na waasi wa zamani wa DRC, Kundi la M23, lililoundwa Mwezi Aprili 2012, lilipata umaarufu wa kimataifa haraka lilipoukalia Mji wa Goma, Mji Mkuu wa Kivu Kaskazini, kwa siku kumi Novemba 2012. Uvamizi huu ulifuatia miezi minane ya mapigano makali katika eneo la Rutshuru. Ingawa waasi hao walijiondoa kutoka Goma baada ya kupata shinikizo kubwa la kimataifa, waliendelea kudhibiti maeneo muhimu ya kimkakati, kama vile mji wa mpakani wa Bunagana.
Baada ya kushindwa na jeshi la DRC Mwaka 2013, M23 ilitia saini makubaliano ya amani na serikali Mwezi Desemba 2013, ambapo ilikubali kuwaondoa wapiganaji wake na kujigeuza kuwa chama cha kisiasa. Hata hivyo, chini ya uongozi wa Kamanda Sultani Makenga, baadhi ya wanachama wa kundi hilo walirejea DRC mwishoni mwa Mwaka 2016, wakiishutumu Serikali ya DRC kwa kushindwa kuheshimu ahadi yake juu ya kuwaondoa wapiganaji wake.
Serikali ya DRC imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23. Rwanda imekuwa ikikanusha tuhuma hizo na badala yake imelishutumu Jeshi la DRC kwa kushirikiana na waasi wa Rwanda wa chama cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kinachofanya kazi Mashariki mwa DRC, ambacho viongozi wao wanalaumiwa kwa mauaji ya kimbari ya Mwaka 1994 dhidi ya Watutsi.
Uhusiano kati ya DRC na Rwanda, ambao ulikuwa umeonyesha dalili za kuimarika chini ya tawala za sasa, sasa uko katika mkwamo wa kidiplomasia, unaosababishwa na kuchochewa na mashambulizi ya hivi karibuni ya M23.
Nchi hizo mbili jirani zina uhusiano tata na uliovurugika tangu mauaji ya kimbari ya Mwaka 1994, baada ya Wahutu wa Rwanda wanaotuhumiwa kuwachinja Watutsi wakati wa mauaji hayo na kuwasili Mashariki mwa DRC.
Hata hivyo, kando na mzozo na majibizano ya kulipizana, nchi hizo mbili pia zinategemea upatanishi wa kikanda na pengine mazungumzo ya kina ya marais wa nchi hizo mbili ambayo hufayika nchini Angola, kujaribu kuzika tofauti na kurejesha amani inayodorora Mashariki mwa DRC.
Lakini hadi leo, mkutano huo bado haupigi hatua kwani hakuna nchi yoyote kati ya hizo mbili ambayo imethibitisha au kutangaza taarifa yoyote ya mkutano huo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma