

Lugha Nyingine
Serikali ya Tanzania yatakiwa kutumia nishati safi kwa magari ili kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni
DAR ES SALAAM - Bunge la Tanzania Alhamisi wiki hii limeitaka serikali ya nchi hiyo kurekebisha magari yake yote kutoka kutumia mafuta hadi kutumia gesi asilia iliyobanwa kwa kushinikizwa (CNG) ili kupunguza uzalishaji wa kaboni na kuokoa gharama za matumizi.
Sillo Baran, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya bajeti, amesema marekebisho ya magari ya serikali pia yatasaidia katika kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje.
Baran amesema licha ya kubarikiwa kuwa na maliasili nyingi ikiwamo gesi asilia, Tanzania iko nyuma katika kutumia rasilimali hizo katika kuchochea maendeleo na kupambana na umaskini.
Mbunge huyo alikuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu hali ya uchumi wa taifa na mpango wa maendeleo wa taifa pamoja na makadirio ya bajeti ya taifa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 yaliyowasilishwa bungeni Jumanne wiki hii.
Amesema nchi nyingi duniani kwa sasa zinahama kutoka kwenye matumizi ya mafuta ya kisukuku kwenda kwenye kutumia nishati mbadala, ikiwa ni pamoja na gesi asilia, ili kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni.
Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam nchini Tanzania (DIT) iliyoko katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam inabadilisha magari kutoka kwenye kutumia petroli hadi kutumia gesi asilia iliyobanwa.
Kwa mujibu wa afisa kutoka DIT, kazi ya urekebishaji ilianza Mwaka 2018 na hadi sasa DIT imebadilisha zaidi ya magari 800 kutoka kwenye matumizi ya mafuta hadi kutumia gesi asilia na watu zaidi wanaendelea kutuma maombi ya kubadilisha mifumo ya nishati ya magari yao.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma