Wataalamu wasema hotuba ya Xi Jinping kwenye Mkuktano wa 25 wa SPIEF inahimiza mshikamano na ustawi wa kimataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 20, 2022

Rais Xi Jinping wa China akihudhuria na kuhutubia kwa njia ya mtandao wa intaneti Mkutano wa 25 wa Baraza la Uchumi la Kimataifa la St.Petersburg, Russia, Juni 17, 2022 (Xinhua/Ju Peng)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping siku ya Ijumaa iliyopita alihutubia Mkutano wa 25 wa Baraza la Uchumi la Kimataifa la St. Peterburg, Russia kwa njia ya mtandao wa intaneti ambapo alitoa mapendekezo manne katika kuhimiza mshikamano na maendeleo endelevu ya kimataifa.

Wataalamu na wasomi kutoka nchi nyingi wanaamini kwamba katika wakati ambapo Dunia inakabiliwa na changamoto nyingi, kauli za Xi zinaongeza nguvu kwa dunia kujenga kwa pamoja siku za baadaye zenye amani, ustawi na mwanga.

Amadou Diop, mtaalamu wa masuala ya China kutoka nchini Senegal, amesema hotuba ya Xi kwa mara nyingine tena imedhihirisha dhamira ya China katika mshikamano wa kimataifa na nia ya nchi hiyo ya kuhimiza ustawi wa pamoja na kudumisha amani duniani.

Cavince Adhere, msomi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa kutoka Nairobi, Kenya, amesema hotuba ya Xi inaakisi matarajio ya nchi nyingi zinazoendelea duniani kote. Ametoa wito kwa nchi za Kusini mwa Dunia kutii wito wa Xi kwa ajili ya kuongeza uratibu na kutafuta suluhisho endelevu kwa changamoto zilizopo.

"Utayari wa Beijing kuhimiza maendeleo yenye ubora wa juu, kupanua ufunguaji mlango kwa kufuata vigezo vya juu, pamoja na kuendeleza ujenzi wa 'Ukanda Mmoja na Njia Mo' unathibitisha nia thabiti ya China ya kubeba wajibu wake wa kimataifa," msomi huyo ameongeza.

Rais Xi Jinping wa China akihudhuria na kuhutubia kwa njia ya mtandao wa intaneti Mkutano wa 25 wa Baraza la Uchumi la Kimataifa la St.Petersburg, Russia, June 17, 2022. (Xinhua/Chen Qiang)

Muhammad Asif Noor, Mkurugenzi wa Taasisi ya Amani na Mafunzo ya Kidiplomasia nchini Pakistan, amesema mapendekezo ya Xi ni yenye haki sana katika kutatua changamoto za pamoja kama vile kutokuwa na uhakika, umaskini, ukosefu wa usawa na misukosuko ya mambo ya fedha inayoikabili jumuiya ya kimataifa.

Ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo na kuongeza misaada kwa nchi nyingine katika miradi ya maendeleo.

Andrei Ostrovsky, Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kijamii na Kiuchumi cha China katika Taasisi ya Mafunzo ya Mashariki ya Mbali chini ya Chuo cha Sayansi cha Russia, amesema China imejitolea kusaidia kujenga uchumi wa Dunia ulio wazi, na kuongeza kuwa chini ya hali ya sasa, Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ni la muhimu sana.

Ahmed Kandil, mtaalam wa Misri wa masuala ya Asia na Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo ya Kimataifa katika Kituo cha Al-Ahram cha Mafunzo ya Kisiasa na Kimkakati, amesema anakubaliana kabisa na pendekezo la Xi la kushirikiana katika uvumbuzi na kufanya matunda ya uvumbuzi kuchangiwa na wote, na kuongeza kwamba sauti ya China ni muhimu inapozungumza kwa ajili ya nchi zinazoendelea.

"Hotuba inatoa wito wa mazungumzo na mabadilishano endelevu kati ya wanafikra, wanasayansi, vituo vya utafiti ili kuelekeza katika kuunda teknolojia mpya zinazosaidia maendeleo ya binadamu na kushinda changamoto na vitisho vinavyoikabili Dunia leo," mtaalamu huyo amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha