Miji mikubwa nchini China yafanya juhudi za kuvutia vipaji vya hali ya juu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 20, 2022

Picha iliyopigwa kutoka angani alfajiri ya Tarehe 1 Aprili 2022 ikionyesha maeneo yaliyo Magharibi mwa Mto Huangpu, Shanghai, Mashariki mwa China. (Picha na Yang Fan/Xinhua)

BEIJING - Miji ya China inafanya juhudi nyingi mpya za kuvutia vipaji kukaa humo, ambazo ni pamoja na hatua zinazofaa kama vile kuondoa mahitaji ya kuwa na usajili wa makazi, kupunguza na kutoa msamaha wa kulipa gharama za kodi za nyumba na hata kutoa ruzuku za kuanzisha biashara na ununuzi wa nyumba.

Mapema mwezi huu, mji mkubwa wa Shanghai ulitangaza kwamba watu waliohitimu kutoka vyuo vikuu 50 bora zaidi duniani wanaorejea katika mji huo wanaweza kusajiliwa moja kwa moja kuwa wakaazi wa mji huo baada ya kuwa waajiriwa wa kudumu katika mji huo, huku hitaji la malipo ya uhakikisho wa kijamii na muda wake wa malipo ukisitishwa.

Ilikuwa ni moja ya hatua zilizoorodheshwa katika notisi inayosisitiza uungaji mkono maalum kwa vipaji iliyotolewa na Ofisi ya Rasilimali Watu na Usalama wa Jamii ya Manispaa ya Shanghai kusaidia kurejesha utendaji kazi na uzalishaji.

Usajili wa makazi, unaoitwa "Hukou" kwa Kichina, daima umekuwa mvuto mkubwa kwa vipaji kwani ndiyo huamua fursa na manufaa kwa mkaazi wa kudumu katika mji husika.

Kwa mujibu wa notisi hiyo, wale waliofuzu kutoka vyuo vikuu bora vilivyoorodheshwa kati ya 51 na 100 duniani kote wanaweza kutuma maombi ya "Hukou" baada ya kufanya kazi ya kudumu Shanghai na kulipa uhakikisho wa kijamii kwa miezi sita, ikiwa ni muda mfupi zaidi kuliko hapo awali.

Wiki iliyopita, mji huo pia ulitangaza sera nzuri mfululizo ikiwa ni pamoja na kupunguza vizuizi vya usajili wa makazi katika maeneo yake mapya ya mijini kwa wahitimu wapya kutoka Shanghai na miji mingine huku ukiongeza muda wa maombi.

Kwa mujibu wa sera hizo, Mwaka 2022, Shanghai itaongeza maeneo 25,000 ya makazi mapya ya kupanga kwa ajili ya vipaji, na kutoa kundi la nyumba za kupangisha za bei nafuu, za muda mrefu na za kudumu kwa wahitimu wapya wanaofanya kazi mjini humo.

Wakati huo huo, kwa ajili ya kurejea kwa kasi katika utendaji kazi na uzalishaji, mji huo pia umefungua "chaneli ya kijani," ikitoa kipaumbele kwa maombi ya kuanzishwa kwa vipaji kutoka kwa makampuni ya biashara muhimu pamoja na wale waliosoma nje ya nchi katika vyuo vikuu mashuhuri.

Wakati Shanghai ikifungua milango yake kwa vipaji, miji mingine ya China pia inashindana kupata wataalamu wenye ujuzi wa kiwango cha juu.

Kituo cha teknolojia ya juu cha Shenzhen kimeongeza ruzuku yake kwa walio na shahada ya udaktari, wenye umri usiozidi miaka 35, hadi kufikia yuan 100,000 (kama dola za Kimarekani 14,942) kwa kila mtu baada ya kuwa mkaazi wa kudumu katika mji huo. Kiasi cha awali cha ruzuku kilikuwa yuan 30,000.

Takwimu za hivi punde kutoka kitengo cha utafiti chini ya Liepin, tovuti ya kutafuta kazi, zinaonyesha kuwa tasnia zinazojumuisha viwanda vinavyotengeneza bidhaa kwa kutumia teknolojia za akili bandia, saketi zilizounganishwa, akili bandia na dawa za kiviumbe hazina wataalamu wa kutosha wenye ujuzi.

Mwaka 2022, China inalenga kutengeneza zaidi ya ajira mpya milioni 11 mijini na kudhibiti ukosefu wa ajira mijini kuwa usiozidi asilimia 5.5.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha