

Lugha Nyingine
Reli ya mwendo kasi ya Beijing-Wuhan yaanza kufanya kazi kwa kasi ya kilomita 350 kwa saa
Picha iliyopigwa kutoka juu ikionyesha treni ya mwendokasi ikienda kwa kasi kwenye reli ya Beijing-Wuhan sehemu ya Reli ya Mwendokasi ya Beijing-Guangzhou, Mjini Wuhan, Mkoa wa Hubei nchini China, Juni 20, 2022. (Xinhua/Xiao Yijiu)
BEIJING - Shirika la Reli la China limesema kuwa reli ya mwendokasi inayounganisha Beijing na Wuhan, mji mkuu wa Mkoa wa Hubei katikati mwa China, imeanza kufanya kazi kawaida kwa kasi ya kilomita 350 kwa saa siku ya Jumatatu.
Kwa mujibu wa shirika hilo, pamoja na kasi ya treni kuongezeka kutoka Kilometa 310 kwa saa hadi Kilomita 350 kwa saa, safari fupi zaidi kati ya Beijing na Wuhan imepunguzwa kwa takriban nusu saa hadi saa tatu na dakika 48.
Shirika hilo limeeleza zaidi kwamba, uwezo wa jumla wa uchukuzi wa sehemu hiyo unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 7, na ongezeko la hadi treni 15 zenye jumla ya siti 18,000 kila siku.
Hivi sasa, China inajivunia kuwa na karibu kilomita 3,200 za reli za mwendokasi ikiwa na kasi ya uendeshaji ya Kilomita 350 kwa saaa, kwenye njia kama vile Reli za Mwendokasi za Beijing-Shanghai, Reli Kati ya miji ya Beijing na Tianjin, na Beijing-Zhangjiakou.
Usalama
Reli ya Beijing-Wuhan ni sehemu ya reli ya mwendokasi ya Beijing-Guangzhou, ambayo iliundwa kufanya safari zake kwa kati ya kilomita 300 kwa saa hadi kilomita 350 kwa saa. Kasi ya kawaida ya uendeshaji wa treni za mwendokasi kwenye laini hiyo iliwekwa kwenye kikomo cha kilomita 310 kwa saa tangu Desemba 2012.
"Usalama ni wa muhimu sana. Tumefanikiwa kufanya majaribio ya mwendokasi kwa takriban kilomita 385 kwa saa na kufanikiwa kabisa kutumia teknolojia ya kuendesha treni za mwendokasi kwa kasi ya kilomita 350 kwa saa," amesema Fu Hong, Mkurugenzi wa Idara ya Matengenezo ya Shirika la Reli la China, Tawi la Beijing.
"Wafanyakazi wa ufundi hufanya kazi ya ukarabati na kuangalia vifaa usiku wa manane na kujaribu mawimbi ya mawasiliano yasiyotumia waya mapema asubuhi," amesema Qiao Zhuyan, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia isiyotumia waya katika shirika hilo. "Kazi hii yote ni kuhakikisha usalama wa operesheni."
Faida
Kama uti wa mgongo wa mtandao wa reli ya mwendokasi katikati mwa China, reli ya Beijing-Wuhan imeunganishwa kwa karibu na reli 12 za mwendokasi nchini humo. Kuongeza kasi yake kuna umuhimu katika kuboresha ufanisi wa mitandao ya reli ya mwendokasi.
Kwa mfano, safari fupi zaidi kutoka Stesheni ya Beijing Magharibi hadi Kituo cha Shijiazhuang, Kituo cha Mashariki cha Zhengzhou, na Kituo cha Wuhan zimepunguzwa hadi saa moja na dakika moja, saa mbili na dakika 11, na saa tatu na dakika 48 mtawalia.
"Kuongeza kasi ya reli hiyo kutasaidia vyema maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya maeneo yaliyoko kando ya reli," amesema Nie Yunfeng anayefanya kazi katika shirika hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma