Marufuku ya Marekani kwa bidhaa kutoka Xinjiang ni mfano wa mabavu ya kiuchumi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 22, 2022

BEIJING - Afisa wa Serikali ya China Jumanne wiki hii alisema kuwa marufuku ya Marekani ya kuagiza bidhaa zote kutoka Mkoa wa Xinjiang wa China ni mfano wa mabavu ya kiuchumi.

Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China alisema kwamba, hatua hiyo itaharibu vibaya maslahi ya wanunuzi wa bidhaa na makampuni ya biashara ya China na Marekani, na haitasaidia kuleta utulivu wa minyororo ya viwanda na ugavi duniani, kupunguza mfumuko wa bei duniani, au kuhimiza ufufuaji wa uchumi wa Dunia.

Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani Jumanne iliweka marufuku ya uagizaji wa bidhaa zote zinazohusiana na Xinjiang, kwa kufuata kile kinachoitwa "Sheria ya Kuzuia Kulazimishwa Kutumikishwa kwa watu wa Kabila la Wauyghur."

Katika kupinga vikali marufuku hiyo, msemaji huyo amesema Marekani inafuata msimamo wa upande mmoja, kujilinda kibiashara na kufanya uonevu kwa jina la "haki za binadamu," hali ambayo inaharibu vibaya kanuni za soko huria na kukiuka sheria za Shirika la Biashara Duniani.

Msemaji huyo akisisitiza kwamba kulazimishwa kutumikishwa kwenye kazi kumepigwa marufuku kwa mujibu wa sheria ya China, makabila yote ya Xinjiang yanafurahia uhuru kamili na fursa sawa katika ajira, na haki na maslahi yao yamehakikishwa ipasavyo.

Kuanzia Mwaka 2014 hadi 2021, mapato halisi ya wakaazi wa mijini katika eneo hilo yaliongezeka kutoka yuan 23,000 (dola za kimarekani 3,440) hadi yuan 37,600, na yale ya wakaazi wa vijijini yalipanda kutoka takriban Yuan 8,700 hadi yuan 15,600. Kufikia mwisho wa Mwaka 2020, zaidi ya watu milioni 3.06 mkoani Xinjiang walikuwa wameondokana na umaskini. Na katika kupanda pamba, moja ya kazi kuu za Xinjiang, kiwango cha kina cha kutumia mashine katika maeneo mengi ya mkoa huo kinazidi asilimia 98.

“Uendelezaji wa kile kinachoitwa kulazimishwa kutumikishwa kwenye kazi hakina msingi hata kidogo, na marufuku ya Marekani itawanyima watu wa Xinjiang haki zao za kufanya kazi na kujiendeleza, na itasababisha ukosefu wa ajira wa kulazimishwa na hata kurudi kwenye umaskini,” Msemaji huyo amesema.

Msemaji huyo amesema kuwa, nia ya kweli ya Marekani ni kuchafua sura ya China, kuingilia mambo yake ya ndani, kuzuia maendeleo yake, na kuleta madhara kwenye ustawi na utulivu wa Xinjiang.

Huku akisisitiza kuwa China itachukua hatua zote za kulipiza, ameitaka Marekani kusitisha mara moja ghiliba zake za kisiasa na kuondoa vikwazo vyote na hatua za ukandamizaji zinazohusiana na Xinjiang. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha