Benki ya Dunia yaidhinisha mpango wa Dola Bilioni 2.3 ili kukabiliana na ukosefu wa usalama wa chakula barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 23, 2022

NAIROBI - Benki ya Dunia Jumatano wiki hii imesema kwamba imeidhinisha mpango wa dola bilioni 2.3 za Marekani ili kusaidia nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kukabiliana na ukosefu wa usalama wa chakula.

Benki ya Dunia imesema fedha hizo zitasaidia kuongeza unyumbulifu wa mifumo ya chakula katika eneo hilo na uwezo wake wa kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa usalama wa chakula.

"Kuhakikisha uratibu wa kikanda katika kushughulikia changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi, hali tete ya soko, na hitaji la marekebisho ya sera za chakula ni vipaumbele muhimu," amesema Hafez Ghanem, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia mambo ya nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, katika taarifa iliyotolewa huko Nairobi, Mji Mkuu wa Kenya.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, inakadiriwa kuwa watu milioni 66.4 katika eneo hilo wanatarajiwa kukumbwa na shinikizo la chakula, au dhiki, hali ya dharura au janga la njaa ifikapo Julai.

Imesema majanga ya mfumo wa chakula yanayosababishwa na hali mbaya ya tabianchi, milipuko ya wadudu na magonjwa, kuyumba kisiasa na kimasoko, na migogoro yanazidi kuwa ya mara kwa mara na ya kutisha, na kuwaweka watu wengi katika hatari ya ukosefu wa usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, mgogoro wa Ukraine unazidisha athari hizi kwa kutatiza soko la kimataifa la chakula, mafuta na mbolea.

Ghanem amesema hii ni operesheni ya kwanza ya kikanda na ya sekta mbalimbali inayolenga kupunguza idadi ya watu wanaokabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa kuongeza unyumbulifu wa mifumo ya chakula na kujiandaa kukabiliana na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama wa chakula.

Amesema nchi za Ethiopia, ambako hadi watu milioni 22.7 hawana usalama wa chakula kutokana na ukame mkali zaidi kuwahi kukabili nchi hiyo, na Madagascar, ambako watu milioni 7.8 wanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa usalama wa chakula kutokana na ukame ambao haujawahi kushuhudiwa kihistoria Kusini mwa nchi hiyo, zitalengwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo.

Awamu ya kwanza pia itasaidia Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD), ambayo itaimarisha upashanaji wa taarifa na takwimu, na Kituo cha Uratibu wa Utafiti wa Kilimo na Maendeleo cha Kusini mwa Afrika, ambacho kitatumia mitandao yake iliyopo na zana za elimu kwa taratibu za uratibu wa kikanda.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha