Rais wa Malawi amzuia Makamu wake kutekeleza majukumu, amfuta kazi mkuu wa polisi kwa tuhuma za ufisadi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 23, 2022

LILONGWE - Rais wa Malawi Lazarus Chakwera Jumanne wiki hii alitangaza uamuzi wa kumzuia Makamu wake Saulos Chilima kutekeleza majukumu yoyote aliyokabidhiwa kufuatia madai ya kiongozi huyo kuhusishwa na ripoti ya ufisadi.

Kiongozi huyo wa Malawi pia amemfukuza kazi Inspekta Jenerali wa Polisi nchini humo George Kainja, na Mkuu wa Watumishi wa Ikulu Prince Kapondamgaga na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Manunuzi na Uondoaji wa Mali za Umma John Suzi Banda kwa sababu hizo hizo za ufisadi.

Katika hotuba kwa taifa iliyotangazwa na televisheni, Rais Chakwera alibainisha kwamba ripoti ya Taasisi ya Kupambana na Rushwa ya Malawi (ACB) imetaja maafisa 84 wa umma wanaoshukiwa kuhongwa na mfanyabiashara wa Uingereza Zuneth Sattar ili kumpendelea kushinda kandarasi za serikali.

Kwa mujibu wa Rais Chakwera, ACB imegundua kuwa Jeshi la Polisi la Malawi na Jeshi la Ulinzi la Malawi yalitoa kandarasi 16 zenye thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 150 kwa kampuni tano za Sattar kati ya Mwaka 2017 na 2021, lakini katika baadhi ya mikataba, serikali ilitapeliwa kwa kulipa “isivyo sawa kwa bei ya juu” ili kununua baadhi ya vifaa.

“Kati ya watu 84 wanaodaiwa kupokea pesa kutoka kwa Sattar Mwaka 2021, 13 wamechunguzwa "kwa mapana" kutokana na kushughulika kifisadi na mfanyabiashara huyo,” Chakwera ameongeza.

Katiba ya Malawi haimruhusu rais kumsimamisha au kumfuta kazi makamu wa rais, hivyo Rais Chakwera amelazimika kuchukua uamuzi wa kumzuia makamu wa rais kuendelea na majukumu aliyokabidhiwa.

Rais amesema, "Kizuri zaidi ninachoweza kufanya kwa sasa, ambacho nimeamua kufanya, ni kumzuia (makamu wa Rais) katika majukumu yoyote aliyokabidhiwa wakati akisubiri Ofisi hiyo ithibitishe tuhuma zake dhidi yake na ijulishe hatua zitakazochukuliwa juu ya jambo hilo."

Wakati huo huo, Chakwera amemuagiza Katibu wa Rais na Baraza la Mawaziri Colleen Zamba kuwachukulia hatua sawa wale wote waliohusishwa na ripoti ya ACB katika wizara, idara na mashirika mbalimbali ya serikali.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha