Ukraine na Russia zabadilishana wafungwa wengi zaidi huku Zelensky akiomba ulinzi kutoka NATO

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 30, 2022

Picha iliyopigwa Tarehe 2 Juni 2022 ikionyesha jengo na lori lililoharibika huko Kharkov, Ukraine. (Picha na Peter Druk/Xinhua)

KIEV – Kurugenzi ya Ujasusi ya Wizara ya Ulinzi ya Ukraine imesema Jumatano wiki hii kwenye mtandao wake wa Telegram kuwa Ukraine na Russia zimefanya mabadilishano ya wafungwa wengi zaidi tangu kuanza kwa mgogoro huo Februari 24 mwaka huu.

Idara hiyo kuu ya ujasusi imesema Wanajeshi 144 wa Ukraine wenye umri wa miaka kati ya 19 na 65 walirudi nyumbani kutokana na kubadilishana.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chini ya mabadilishano hayo, Russia iliachilia huru wanajeshi 59 wa Jeshi la Ulinzi wa Taifa la Ukraine, wakiwemo 43 wa kikosi cha Azov kilichopigania kiwanda cha chuma cha Azovstal huko Mariupol.

“Wengi wa wapiganaji wa Ukraine walioachiliwa wana majeraha mabaya,” imesema taarifa hiyo.

Ukraine na Russia zilifanya mabadilishano ya kwanza ya wafungwa Machi 24.

Wakati hayo yakiwa yameripotiwa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Jumatano wiki hii alihutubia mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) kupitia njia ya video, akihimiza msaada zaidi wa ulinzi na kifedha kwa Ukraine.

Katika hotuba yake, Zelensky alisema kuwa Ukraine inahitaji makombora na mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga ili kulinda miji yake, na mizinga kwa ajili ya kukabiliana na Russia kwenye medani za vita.

"Tunahitaji hakikisho la usalama, na inabidi mtafute nafasi ya Ukraine kwenye sehemu ya usalama wa pamoja," Zelensky alisisitiza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha