Nchi za Umoja wa Forodha Kusini mwa Afrika zakabiliwa na hatari kubwa ya kudorora kiuchumi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 01, 2022

Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi akihutubia Mkutano wa 7 wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Forodha wa Kusini mwa Afrika (SACU) mjini Gaborone, Botswana, Juni 30, 2022. Rais Mokgweetsi Masisi wa Botswana Alhamisi wiki hii amesema nchi za SACU, ambazo ni Botswana, Afrika Kusini, Eswatini, Namibia na Lesotho, sasa ziko katika kipindi ambacho hatari ya kudorora kiuchumi inaongezeka. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

GABORONE - Rais Mokgweetsi Masisi wa Botswana Alhamisi wiki hii amesema nchi za Umoja wa Forodha wa Kusini mwa Afrika (SACU), ambazo ni Botswana, Afrika Kusini, Eswatini, Namibia na Lesotho, sasa ziko katika kipindi ambacho hatari ya kudorora kiuchumi inaongezeka.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa 7 wa wakuu wa nchi na serikali wa SACU huko Gaborone, Mji Mkuu wa Botswana, Masisi amesema mgogoro unaoendelea kati ya Russia na Ukraine unafifisha matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa kiwango ambacho ukuaji unakadiriwa utapungua hadi asilimia 3.6 Mwaka 2022.

"Sasa tuko katika kipindi ambacho kuna kuongezeka kwa hatari ya kudorora kiuchumi," amesema Masisi, na kuongeza kuwa makadirio ya ukuaji wa uchumi kwa Mwaka 2022 yanafikia asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 6.8 Mwaka 2021 na makadirio ya kuimarika kwa hadi asilimia 4.4 Mwaka 2023.

Masisi amesema mgogoro kati ya Russia na Ukraine umezidisha hali ya uchumi ambayo tayari imeshuka kutokana na athari za janga la UVIKO-19 pamoja na usumbufu kwenye minyororo ya kimataifa ya ugavi, na hivyo kusababisha kuongezeka kwa mfumuko wa bei duniani kote, ikiwemo ukanda wa SACU.

Kwa mujibu wa Masisi, ongezeko la mfumuko wa bei, hasa kwa chakula na nishati, bado ni hatari iliyopo sasa duniani ambayo inaumiza wanunuzi wa bidhaa na kudhoofisha uwezo wao wa kununua.

“Hii inatoa wito kwa nchi za SACU kuchukua hatua za kukabiliana na hali ya kiuchumi ili kuinua uchumi wao,” amesema Masisi.

Zaidi ya hayo, Masisi amesema kudorora kwa uchumi katika ukanda wa SACU kunadhihirisha umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa mipango ya kufufua uchumi wa nchi husika na kuendelea kuhamasisha ufadhili unaohitajika.

Naye Katibu Mtendaji wa SACU, Paulina Elago amesema umoja huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda kupitia maendeleo ya minyororo ya thamani ya kikanda katika usindikaji wa mazao ya kilimo, mavazi na nguo, vipodozi na mafuta muhimu pamoja na dawa.

SACU iliyoanzishwa Mwaka 1910, ndiyo muungano wa zamani zaidi wa forodha duniani na makao yake makuu yapo katika mji mkuu wa Namibia, Windhoek.

Paulina Elago (Kulia), Katibu Mtendaji wa Umoja wa Forodha wa Kusini mwa Afrika (SACU), akizungumza kwenye Mkutano wa 7 wa wakuu wa nchi na serikali wa SACU huko Gaborone, Botswana, Juni 30, 2022. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

Picha iliyopigwa Juni 30, 2022 ikionyesha eneo la Mkutano wa 7 wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Forodha wa Kusini mwa Afrika (SACU) huko Gaborone, Botswana. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha