

Lugha Nyingine
Uganda yapitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya taifa
KAMPALA – Serikali ya Uganda imetangaza kupitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya taifa.
Waziri wa Teknolojia ya Mawasiliano na Mwongozo wa Taifa wa Uganda Chris Baryomunsi, amewaambia waandishi wa habari Jumanne wiki hii kwamba Baraza la Mawaziri la nchi hiyo Jumatatu liliidhinisha utekelezaji wa agizo la Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwamba Kiswahili kipitishwe kuwa lugha rasmi ya jumuiya hiyo. Uganda sasa ina lugha mbili rasmi, Kiingereza na Kiswahili.
EAC inaziunganisha nchi saba wanachama ambazo ni Uganda, Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Baryomunsi amesema Baraza la Mawaziri la Uganda pia liliagiza kwamba masomo ya lugha ya Kiswahili na mitihani yake katika shule za msingi na sekondari iwe lazima.
Ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200, Lugha ya Kiswahili inayotokea Afrika Mashariki, ni mojawapo ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani.
Katika mkutano wake wa hivi karibuni wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), lugha hiyo ilipitishwa kuwa lugha rasmi ya kazi.
Mwaka 2019, Kiswahili kilipitishwa kuwa lugha pekee yenye asili ya Afrika inayotambuliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Muda mfupi baadaye, ilianza kufundishwa katika shule kote nchini Afrika Kusini na Botswana.
Hivi majuzi, Chuo Kikuu cha Addis Ababa cha Ethiopia kilitangaza kitaanza kufundisha Kiswahili.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), hivi majuzi liliteua Tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya Lugha ya Kiswahili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma