

Lugha Nyingine
Rais wa Afrika Kusini awaonya raia dhidi ya unywaji pombe katika umri mdogo
CAPE TOWN - Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Jumatano wiki hii amewaonya raia dhidi ya unywaji pombe katika umri mdogo, akisema nchi hiyo inapoteza kizazi chake cha baadaye kutokana na "janga hili."
Ametoa onyo hilo kwenye mazishi ya halaiki ya vijana 21 waliofariki kutokana na tukio lililotokea kwenye klabu ya usiku wiki iliyopita huko East London, Jimbo la Eastern Cape. Mwathiriwa mdogo aliyekufa katika janga hilo alikuwa na umri wa miaka 13, na nchi hiyo bado inangojea matokeo ya vipimo vya sumu.
Umri halali wa mtu kuruhusiwa kunywa pombe nchini Afrika Kusini ni miaka 18.
Ramaphosa amekumbuka matukio makubwa yanayohusiana na unywaji pombe ambayo yaliua vijana wanawake na watoto siku za nyuma, akilaumu unywaji pombe katika umri mdogo kwa kusababisha ukatili unaohusiana na pombe, ajali za barabarani, watu kuendesha gari wakiwa wamelewa na kufanya ngono zisizo salama.
"Pombe ina uraibu wa hali ya juu. Ni kitu cha kunywewa kwa kiasi na kwa uwajibikaji, na ni kwa wale tu walio katika umri halali kufanya hivyo, na waliokomaa vya kutosha kushughulikia athari zake," amesema.
Ramaphosa amesema Afrika Kusini ina sheria nyingi za kushughulikia na kupambana na matumizi mabaya ya pombe, lakini inabidi kuimarisha utekelezaji, akitoa wito kwa mameya wote kuteua Kamati za Mitaa za Kupambana na Dawa za Kulevya katika kila kata na kuzipa msaada unaohitajika kutoka kwa manispaa.
Pia ametoa wito kwa serikali ya Eastern Cape na serikali zote za majimbo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango mikuu yao ya dawa za kulevya, kwa kuzingatia upya utoaji elimu na uhamasishaji wa umma.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma