

Lugha Nyingine
China yatangaza tena tahadhari ya rangi ya chungwa kwa halijoto ya juu
Mtu akitembea karibu na chemchemi huku kukiwa na joto kali katika Eneo la Minhang, huko Shanghai, Mashariki mwa China, Julai 10, 2022. (Xinhua/Fang Zhe)
BEIJING - Idara ya uchunguzi wa hali ya hewa ya China siku ya Jumapili iliendelea kutoa tahadhari ya rangi ya chungwa kuhusu joto la juu huku mawimbi makali ya joto yakiendelea katika maeneo mengi ya nchi hiyo.
Kituo cha Hali ya Hewa cha China kimesema, wakati wa mchana siku ya leo Jumatatu, baadhi ya sehemu za mikoa ya Zhejiang, Fujian, Jiangxi, Hunan, Guangdong, Guangxi, Guizhou, Sichuan, Chongqing, Hubei, Jiangsu, Anhui, Inner Mongolia na Xinjiang zinatarajiwa kupata joto la zaidi ya nyuzi joto 35.
“Joto katika baadhi ya sehemu za mikoa ya Zhejiang, Fujian, Jiangxi na Xinjiang huenda likapita nyuzi joto 40,” kituo hicho kimesema.
Kituo hicho kimewashauri wananchi kuepuka shughuli za nje wakati wa kuwa na joto kali na kupendekeza kuwa wafanyakazi walio kwenye joto la juu wapunguze muda wa kufanya kazi mfululizo.
China ina mfumo wa tahadhari ya hali ya hewa wenye hatua nne, unaowakilishwa kwa alama za rangi, na rangi nyekundu inaashilia tahadhari kali zaidi, ikifuatiwa na machungwa, manjano na buluu.
Wiki mbili zilizopita, Idara ya hali ya hewa ya Shanghai, China ilitoa tahadhari nyekundu ya joto kali huku halijoto katika baadhi ya maeneo ya mji huo ikipanda hadi nyuzi joto 40.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma