

Lugha Nyingine
Washirika wa Misaada ya kibinadamu waweza kusitisha msaada kwa Somalia kutokana na ukosefu wa fedha
MOGADISHU - Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) Jumapili imeonya kuwa washirika wa misaada ya kibinadamu watalazimika kusitisha miradi muhimu ya misaada kwa Somalia kutokana na ukosefu wa fedha.
OCHA imesema bila ufadhili wa haraka, miradi hiyo ikiwemo msaada wa chakula, shughuli za lishe, utoaji wa huduma bora za afya na usaidizi wa kimaisha itasitishwa.
"Wasomali zaidi watateseka, na maendeleo yaliyopatikana katika muongo uliopita yatapotea," OCHA imesema katika ripoti yake ya hivi punde kuhusu gharama ya kutochukua hatua iliyotolewa huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba hali ya dharura ya ukame nchini Somalia imezidi kuwa mbaya huku karibu nusu ya watu nchini Somalia, takribani milioni 7.7, wakihitaji msaada wa kibinadamu au ulinzi.
Imesema ukame umeathiri watu wasiopungua milioni 7, kati yao, watu 918,000 wamekimbia makazi yao kutafuta maji, chakula na malisho, ikiwa ni pamoja na makundi ya jamii za walio wachache.
"Nchi inakabiliwa na uwezekano mkubwa wa njaa katika wilaya 17 ikiwa uzalishaji wa mazao na mifugo utashindwa, bei ya chakula itaendelea kupanda na misaada ya kibinadamu haitadumishwa ili kufikia watu walio hatarini zaidi," OCHA imesema.
Umoja wa Mataifa umeonya hapo awali kwamba hatua za haraka zinahitajika ili kuongeza na kudumisha misaada ya kibinadamu, angalau hadi mwisho wa Mwaka 2022, ili kuzuia kuongezeka kwa viwango vya ukosefu wa usalama wa chakula, kupunguza watu kupoteza maisha, na kuepusha hatari ya njaa.
"Bila ya kuongeza misaada, ukame utasababisha watu wengi kuhama makazi yao, magonjwa ya kuambukiza na ukiukaji wa ulinzi nchini Somalia," OCHA imeonya.
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba misimu minne mfululizo ya mvua iliyoshindwa ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo, kupanda kwa bei na kukosekana kwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu kumesababisha ongezeko la watu wanaokabiliwa na viwango vya janga la ukosefu wa usalama wa chakula, njaa na magonjwa nchini Somalia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma