Rais Xi Jinping azungumza na Joe Biden kwa njia ya simu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 29, 2022

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping Alhamisi jioni alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Joe Biden. Marais hao wawili walibadilishana maoni kwa uwazi kuhusu uhusiano kati ya China na Marekani na masuala yanayofuatiliwa na pande hizi mbili.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa ombi la Rais Biden, Xi ameweka bayana kuwa katika Dunia ya sasa, mwelekeo wa misukosuko na mageuzi unazidi kubadilika, na nakisi katika maendeleo na usalama inaonekana wazi. Ikikabiliwa na mabadiliko na machafuko yaliyotokea duniani, jumuiya ya kimataifa na watu duniani kote wanatarajia China na Marekani zichukue nafasi ya mbele katika kudumisha amani na usalama wa Dunia na kuhimiza maendeleo na ustawi wa Dunia. Huu ni wajibu wa China na Marekani ambazo ni nchi mbili kubwa.

Amesisitiza kuwa kuutazama na kuufafanua uhusiano kati ya China na Marekani kutoka kwa mrengo wa ushindani wa kimkakati na kuiona China kama mpinzani mkuu na changamoto kubwa zaidi ya muda mrefu, itakuwa kutouelewa uhusiano kati ya China na Marekani na kuyaelewa vibaya maendeleo ya China, na itakukwa ni kuwapotosha watu wa nchi hizo mbili na jumuiya ya kimataifa. “Pande hizo mbili zinahitaji kudumisha mawasiliano katika ngazi zote na kutumia vyema njia zilizopo za mawasiliano ili kuhimiza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.” Rais Xi amesema

Akitambua changamoto nyingi zinazoukabili uchumi wa Dunia, Xi amesisitiza haja ya China na Marekani kudumisha mawasiliano katika masuala muhimu kama vile kuratibu sera za uchumi wa jumla, kuweka minyororo ya kimataifa ya viwanda na ugavi katika uimara, na kulinda nishati na usalama wa chakula duniani. Amesema, majaribio ya kutenganisha au kukata minyororo ya ugavi kinyume na sheria za msingi haitasaidia kukuza uchumi wa Marekani. Itafanya tu uchumi wa Dunia kuwa hatarini zaidi.

Amesema pande hizo mbili zinahitaji kushirikiana katika kupunguza hatari ya kupamba moto kwa migogoro ya kikanda, kusaidia kuiepusha Dunia na UVIKO-19 mapema iwezekanavyo, kupunguza hatari ya kudorora na kushuka kwa uchumi, na kulinda mfumo wa kimataifa na Umoja wa Mataifa ukiwa katika msingi wake na mfumo wa utaratibu wa kimataifa unaoungwa mkono na sheria za kimataifa.

Xi pia amezungumzia suala la Taiwan, akifafanua msimamo wa China kuhusu Taiwan. Amesisitiza kwamba muktadha wa kihistoria wa suala la Taiwan uko wazi kabisa, na ndivyo ukweli na hali ilivyo kwamba pande zote mbili za Mlango-Bahari wa Taiwan ni za China moja.

Alisema, msimamo wa Serikali ya China na watu wake kuhusu suala la Taiwan ni thabiti, na kulinda kwa uthabiti mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi ya China ni dhamira thabiti ya watu zaidi ya bilioni 1.4 wa China.

Xi ameitaka Marekani kuheshimu kanuni ya kuwepo kwa China moja na kutekeleza masharti yaliyoko kwenye nyaraka tatu za makubaliano ya pamoja kati China na Marekani huku akiongeza kuwa, inatarajiwa Marekani itakuwa na muono sahihi kuhusu hili.

Kwa upande wake, Rais Biden amesema Dunia iko katika wakati mgumu, na kuongeza kuwa ushirikiano wa Marekani na China unanufaisha siyo tu watu wa nchi hizo mbili, bali pia watu wa nchi zote.

Amesema Marekani inatarajia kuweka njia wazi ya mawasiliano na China ili kuongeza maelewano na kuepuka dhana potofu na makosa yasiyotarajiwa katika maamuzi, na itashirikiana na China ambapo maslahi ya nchi hizo mbili yanapatana, wakati huo huo, kusimamia ipasavyo tofauti.

Amesisitiza kuwa sera ya Marekani kuhusu kuwepo kwa China moja haijabadilika na haitabadilika, na kwamba Marekani haiungi mkono " Taiwan ijitenge ."

Marais hao wawili pia wamebadilishana mawazo kuhusu masuala kadhaa ya kimataifa na kikanda, yakiwemo mgogoro wa Ukraine. Katika hili Xi amesisitiza msimamo wa China.

Marais wote wawili wameona mawasiliano yao hayo ya simu yalikuwa ya wazi na ya kina. Wamekubaliana kuendelea kuwasiliana na kuagiza maofisa wa nchi hizo mbili kuendelea na mawasiliano na ushirikiano.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha