China imetoa taarifa kupitia idara zake mbalimbali ikilaani na kupinga vikali ziara ya Pelosi kisiwani Taiwan

(CRI Online) Agosti 03, 2022

Idara mbalimbali za China jana Jumanne zilitoa taarifa ya kupinga na kulaani vikali ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi katika kisiwa cha Taiwan cha China, kwa kupuuza maonyo makali yaliyotolewa na China.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema ziara ya Pelosi imekiuka vibaya kanuni ya China moja na taarifa tatu za pamoja kati ya China na Marekani pia imetuma "ishara zisizo sahihi" kwa makundi ya ufarakanishaji yanayotaka "Taiwan ijitenge". Aidha imesisitiza kuwa duniani kuna China moja tu, Taiwan ni eneo lisiloweza kutengwa la China, na serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ndio serikali kuu halali inayowakilisha China nzima.

China na Marekani ni nchi mbili kubwa, hivyo njia sahihi ya kushughulikia masuala yao ipo kwenye kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani, kutokabiliana na kuwa na ushirikiano wa kunufaishana. Hivyo imekumbusha Marekani kwamba suala la Taiwan ni mambo ya ndani ya China, na hakuna nchi nyingine yenye haki ya kujifanya kama hakimu kwenye suala la Taiwan. China pia inaitaka Marekani kuacha kutumia “karata ya Taiwan” na kuitumia Taiwan yenyewe kuidhibiti China.

Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge la Umma la China kupitia msemaji wake imelaani ziara ya Pelosi ikisema imedhoofisha vibaya mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi wa China, na kuathiri vibaya msingi wa siasa kwenye uhusiano wa China na Marekani.

Imesema Marekani imeiahidi China juu ya suala la Taiwan, lakini kivitendo mara kwa mara imekuwa ikiongeza uhusiano wake na Taiwan na maofisa wa pande mbili kuwasiliana, kutia moyo na kuunga mkono makundi ya ufarakanishaji yanayotaka “Taiwan ijitenge” na kujaribu kuitumia Taiwan kwa kuidhibiti China, pamoja na kudhoofisha vibaya amani na utulivu wa mlango bahari wa Taiwan.

Kwa upande wake Ofisi ya Kazi ya Taiwan ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China CPC imesema ziara ya Pelosi kisiwani Taiwan imeonesha kuongezeka kwa ushirikiano kati ya Marekani na mkoa wa Taiwan, hatua ambayo inaonesha nia mbaya kupindukia na ina matokeo makubwa. Imesema kanuni ya kuwepo kwa China moja ni kanuni inayotambulika katika uhusiano wa kimataifa na imekubaliwa na jumuiya ya kimataifa.

Sambamba na hilo, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China Wu Qiang naye amesema watawala wa Chama cha Maendeleo ya Kidemokrasia cha Taiwan wanaomba uungaji mkono kutoka nje, kushirikiana na makundi ya nje kuchochea matatizo na zimekuwa zikilazimisha kumualika Pelosi kutembelea Taiwan. Amesema kitendo kama hicho ni hatari sana na kitapeleka matokeo makubwa. Jeshi la Ukomboza wa Umma la China lipo kwenye tahadhari kubwa na litafanya operesheni kubwa katika kulinda mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi wa China. Nayo Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la mashauriano ya Kisiasa la Umma la China pia imelaani vikali ziara ya Pelosi kisiwani Taiwan.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha