

Lugha Nyingine
Watu 52 wafariki kutokana na mvua nchini Sudan
KHARTOUM – Serikali ya Sudan jana Jumapili imetoa taarifa kwamba, takriban watu 52 wameuawa na wengine 25 kujeruhiwa wakati mvua kubwa iliponyesha kote nchini humo.
“Miongoni mwa waliofariki ni watu 19 walioripotiwa katika Jimbo la Kordofan Kaskazini katikati mwa Sudan,” Baraza la Taifa la Ulinzi wa Raia la nchi hiyo limetoa taarifa kupitia kwenye tovuti yake.
Taarifa hiyo imesema kuwa, hekta 219 za ardhi ya kilimo zilifurika maji, nyumba 5,345 zimebomolewa na 2,862 kuharibika wakati wa msimu wa wa sasa wa mvua kote nchini humo.
“Jimbo la Mto Nile Kaskazini ni miongoni mwa majimbo yaliyoathirika zaidi, na jumla ya nyumba 2,732 zimebomolewa na takriban 690 kuharibiwa,” imeongeza taarifa hiyo.
Msemaji wa baraza hilo Abdul-Jalil Abdul-Rahim amewataka wananchi kuacha kujenga karibu na mito au kwenye vijito na kufuata maelekezo rasmi.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi la Ulinzi wa Raia la Sudan limesema kuwa misafara iliyobeba vifaa vya malazi, ikiwa ni pamoja na mablanketi, mahema na pampu za maji, imetumwa katika Jimbo la Mto Nile na majimbo yaliyoathiriwa Magharibi mwa Sudan.
Awad Ibrahim, mtaalamu wa hali ya hewa wa eneo hilo, amewataka watu kuchukua tahadhari kwani kuna tahadhari ya mvua kubwa zaidi wiki hii katika maeneo mengi ya Sudan huku mawingu ya cumulus yakisonga mbele kutoka nyanda za juu za Ethiopia Mashariki.
Sudan mara nyingi hushuhudia mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa kuanzia miezi ya Juni hadi Oktoba.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma