

Lugha Nyingine
Ethiopia yazindua mradi mkubwa wa barabara zilizojengwa na China katika mji mkuu Addis Ababa
ADDIS ABABA - Ethiopia siku ya Jumatatu ilizindua mradi mkubwa wa barabara uliojengwa na China katika mji mkuu wa Addis Ababa.
Mradi wa Barabara ya Makutano wa Alexander Pushkin Square-Gotera, ambao ni barabara ya kilomita 3.8 inayojumuisha sehemu tatu na ujenzi wa handaki lenye njia mbili za urefu wa mita 320, kandarasi yake ilipewa kampuni ya China First Highway Engineering (CFHEC).
Adanech Abiebie, Meya wa Mji wa Addis Ababa, amesema kwenye uzinduzi wa mradi wa barabara hiyo kwamba mradi huo ni uthibitisho wa kujitolea kwa Ethiopia katika kufanya miradi muhimu ya maendeleo katika muda mfupi na ubora wa juu.
"Mradi huu wa barabara, pamoja na kutoa mfano mzuri wa utekelezaji bora wa mradi wa barabara kwa mji na nchi yetu, pia utaboresha kwa kiasi kikubwa safari za magari katika sehemu hii ya mji yenye msongamano mkubwa," Abiebie amesema.
"Tungependa kuwashukuru Serikali ya China na watu wake kwa mradi huu mzuri, pia kwa kufadhili na kutekeleza mradi," meya huyo ameongeza.
Amesisitiza zaidi kwamba mradi huo mpya wa barabara uliozinduliwa siyo tu utapunguza msongamano wa magari katika mazingira yake lakini pia utaongeza uzuri mwingine wa eneo hilo.
Kukamilika kwa mradi huo kwa wakati, ambao ulianza kwa tukio la kuwekwa jiwe la msingi mnamo Oktoba 2019, inasemekana kuwa hatua nyingine muhimu ambayo ni mfano wa miradi mikubwa kama hiyo ya maendeleo katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Shen Qinmin, Kaimu Balozi wa China nchini Ethiopia, amesema Mradi wa Barabara ya Juu ya Alexander Pushkin Square-Gotera, ni ishara ya ushirikiano na urafiki kati ya China na Ethiopia.
Shen amesema China na Ethiopia ni ndugu wa nyakati zote. Amesema nchi hizo mbili zimepitisha mikakati ya maendeleo inayoshabihiana sana, na kufanya ushirikiano wenye tija unaoweka kasi ya ushirikiano kati ya China na Afrika kwa ujumla.
"China kama nchi inayoendelea inaelewa kikamilifu mahitaji na matarajio ya watu wa Ethiopia na serikali. Tunajua jinsi barabara au miundombinu ilivyo muhimu kwa kutimiza ndoto za taifa na maendeleo ya kiuchumi pia," amesema.
Amethibitisha kuwa China inaendelea kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo wa Ethiopia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma