Waziri Mkuu wa Tanzania awataka Wakuu wa Mikoa kutatua changamoto zinazolikabili zoezi la sensa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 26, 2022

DAR ES SALAAM - Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Alhamisi wiki hii amewataka wakuu wa mikoa kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi iliyoanza Jumanne wiki hii.

“Kila mkoa unapaswa kukusanya takwimu za sensa ifikapo saa nane mchana kila siku, hii itasaidia kubaini mapungufu yanayokabili zoezi hilo na kuyatatua,” amesema Majaliwa kwenye mkutano na wakuu hao wa mikoa uliofanyika kwa njia ya video.

Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi nchini Tanzania ilianza Agosti 23 na itafanyika kwa siku saba hadi Agosti 29.

Majaliwa amesema kamati za sensa za wilaya na mikoa zinapaswa kufuatilia kila mara jinsi sensa inavyoendelea kufanyika ili kuhakikisha watanzania wote wanahesabiwa.

Albina Chuwa, Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), amesema kaya 5,060,158 zenye watu 22,004,910 zimehesabiwa hadi kufikia Alhamisi asubuhi.

Akihutubia Taifa Jumatatu usiku kuelekea Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania aliwataka Watanzania wote kujitokeza kushiriki kwenye sensa hiyo ili kuwezesha nchi hiyo kuwa na takwimu stahiki zitakazosaidia katika kupanga mipango ya maendeleo.

"Takwimu bora zitasaidia nchi yetu kupanga maisha bora na uwajibikaji," alisisitiza.

Rais Samia alisema matokeo ya awali ya sensa yatatangazwa Mwezi Oktoba.

Sensa ya mwisho ya watu na makazi ilifanyika Tanzania Mwaka 2012.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha