

Lugha Nyingine
Makumi ya wasafiri watekwa nyara na watu wenye silaha Kusini mwa Nigeria
ABUJA - Polisi nchini Nigeria siku ya Jumapili wamesema wameanzisha msako wa kuwatafuta watu wenye silaha ambao walishambulia mabasi yaliyokuwa yakisafirisha baadhi ya wasafiri katika sehemu ya Kusini mwa nchi hiyo, na kuwateka makumi ya watu hao siku ya Jumamosi.
Msemaji wa polisi huko Ondo, Funmilayo Ibukun Odunlami ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwa njia ya simu kwamba, baadhi ya waathirika wa tukio hilo lililotokea karibu na Ifon, mji ulio kando ya barabara ya Benin-Owo, Jimbo la Ondo, Kusini Magharibi mwa nchi hiyo waliokolewa Jumapili alasiri na timu ya polisi.
"Ninaweza kukuthibitishia kwamba baadhi ya waathiriwa waliokolewa wakati wa operesheni ya polisi leo (Jumapili) mchana. Lakini siwezi kutoa idadi kamili ya waliookolewa sasa kwa sababu watu wetu bado wanafanya kazi ya kuwaokoa wengine," Odunlami amesema.
Kwa mujibu wake, idadi ya wasafiri waliotekwa nyara na watu hao wenye silaha bado haijajulikana, kwani oparesheni ya uokoaji ilikuwa bado inaendelea.
Watu hao wenye silaha waliibuka kutoka msituni huko Ifon Jumamosi jioni, wakati mabasi mawili yaliyokuwa yamepakia abiria kutoka jimbo jirani la Edo kwenda Ondo yaliposafiri kupitia njia hiyo, vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti Jumapili, na kuongeza kuwa takribani wasafiri 32, ambao walikuwa wametoka kuhudhuria mazishi huko Edo wametekwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma