Rais Xi wa China aagiza kufanya juhudi zote za uokoaji baada ya tetemeko la ardhi kutokea Kusini Magharibi mwa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 06, 2022

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ameagiza kufanya juhudi zote za uokoaji baada ya tetemeko la ardhi lenye kipimo cha Ritcher 6.8 kuukumba Mkoa wa Sichuan, Kusini Magharibi mwa China siku ya Jumatatu, huku akisisitiza kwamba kuokoa maisha inapaswa kuchukuliwa kama jukumu la msingi.

Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC), ametoa maagizo hayo baada ya tetemeko hilo kutokea katika eneo la wilaya ya Luding ya Tarafa inayojiendesha ya Watibet ya Ganzi , saa 12:52 jioni Jumatatu.

Tetemeko hilo la ardhi hadi sasa limesababisha vifo vya watu wasiopungua 21 na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya maji na umeme, usafiri na mawasiliano.

Xi amesisitiza kuimarisha ufuatiliaji wa tetemeko, kujilinda dhidi ya majanga ya pili, na kuwahudumia ipasavyo wale walioathiriwa.

Huku akitoa wito wa kufanywa kwa juhudi kubwa za kuhakikisha usalama wa maisha na mali za watu, Xi ameiagiza Wizara ya Usimamizi wa Dharura na idara nyingine za Serikali ya China kutuma timu huko Sichuan ili kuongoza kazi ya kutoa misaada na kuagiza Jeshi la Ukombozi wa Umma na Jeshi la Polisi la Umma la China kusaidia kikamilifu juhudi za serikali za mitaa za kukabiliana na maafa hayo.

Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang, pia amehimiza kuthibitisha haraka hali halisi ya athari ya maafa, pamoja na kuharakisha juhudi za uokoaji na matibabu.

Pia amewataka wakazi wa eneo hilo kukaa macho dhidi ya majanga ya pili kama vile maporomoko ya ardhi, kuongeza juhudi za kuwapokea wale wanaotoka katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi, na kukarabati kwa haraka miundombinu ya usafiri na mawasiliano ya simu haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa maagizo ya Xi na Li, idara zote husika zikiwemo Wizara ya Usimamizi wa Dharura, Wizara ya Maliasili na Kamati ya Taifa ya Afya ya China zimetuma timu kwenye maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi ili kutoa mwelekeo kuhusu misaada ya kukabiliana na maafa.

Serikali ya Mkoa wa Sichuan na Wilaya ya Luding ya Tarafa inayojiendesha ya Watibet ya Ganzi zimepanga wafanyakazi kutekeleza misheni ya kutoa misaada ya maafa na kupeleka mahema, vifaa vya malazi na rasilimali nyingine kwenye maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha