Rais Xi wa China asisitiza kuboresha mfumo wa kufikia mafanikio kwenye teknolojia za msingi katika nyanja muhimu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 07, 2022

BEIJING - Rais Xi Jinping wa China Jumanne wiki hii amesisitiza kuboresha mfumo mpya wa kuhamasisha rasilimali za nchi nzima ya China ili kufikia mafanikio kwenye teknolojia za msingi katika nyanja muhimu na kuimarisha juhudi za kuhifadhi rasilimali.

Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC) ameyasema hayo wakati akiongoza mkutano wa 27 wa Kamati Kuu ya Mageuzi ya Kina ya China.

Katika mkutano huo, kamati ilipitia na kupitisha mwongozo wa kuboresha mfumo mpya wa kuhamasisha rasilimali nchi nzima ili kufikia mafanikio katika teknolojia za msingi katika nyanja muhimu chini ya uchumi wa kijamaa wa soko, mwongozo wa kuimarisha mageuzi ya mfumo wa kitaaluma, mwongozo wa kuimarisha kazi ya kubana matumizi ya maliasili, mwongozo wa kuimarisha majaribio ya uuzaji wa ardhi ya pamoja ya vijijini iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi unaohusiana na biashara, na mwongozo wa kuimarisha mageuzi ili kuhimiza maendeleo mazuri ya mfumo wa matibabu na afya vijijini.

Xi, ambaye pia ni mkuu wa kamati hiyo, amesema China inapaswa kutumia nguvu bora za mfumo wa ujamaa ambao una uwezo wa kukusanya rasilimali ili kukamilisha mipango muhimu, kuimarisha uongozi wa CPC na serikali juu ya uvumbuzi mkubwa wa kisayansi na kiteknolojia, na kutoa mchango kamili kwenye jukumu la soko.

“China inapaswa kuboresha ugawaji na uvumbuzi wa raslimali kwa kuzingatia mahitaji ya kimkakati ya nchi, kuimarisha nguvu za kimkakati za kisayansi na kiteknolojia, kuboresha kwa kiasi kikubwa uwezo wa kimfumo wa kushughulikia changamoto kuu za kisayansi na kiteknolojia, kuongeza uwezo wa ushindani na kunyakua mpango wa kimkakati katika maeneo muhimu,” Xi amesema.

Pia amesisitiza juhudi za kuimarisha mageuzi ili kutoa nafasi ya ushiriki bora wa wasomi.

“Nchi inapaswa kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali katika nishati, maji, nafaka, ardhi, madini na malighafi, na kuharakisha mabadiliko ya kimsingi ya mbinu za matumizi ya rasilimali,” Xi amesema.

Kuhusu masuala ya vijijini, Xi amesisitiza juhudi za kuhimiza mpango wa majaribio wa uuzaji wa ardhi ya pamoja ya vijijini iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi unaohusiana na biashara, na kuendeleza mfumo wa matibabu na afya wa vijijini ambao una ufanisi mkubwa na unaokubalika kwa umaalumu wa vijijini.

Li Keqiang, Wang Huning na Han Zheng, ambao wote ni wajumbe wa kudumu wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC na manaibu wakuu wa kamati hiyo, wamehudhuria kwenye mkutano huo.

Mkutano huo pia umetoa wito wa kuendeleza utafiti kuhusu teknolojia muhimu zenye manufaa ya kwanza, na kuhusu teknolojia za kisasa ambazo zitaongoza maendeleo ya baadaye.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha