Rais Xi Jinping asema China iko tayari kushirikiana na kusaidiana na Russia katika masuala yanayohusu maslahi ya msingi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 16, 2022

Rais wa China Xi Jinping akikutana na Rais wa Russia Vladimir Putin kwenye ukumbi wa Forumlar Majmuasi huko Samarkand, Uzbekistan, Septemba 15, 2022. Xi amekutana na Putin mjini Samarkand ili kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano kati ya China na Russia na masuala ya kimataifa na kikanda yenye maslahi ya pamoja. (Xinhua/Ju Peng)

SAMARKAND, Uzbekistan - China iko tayari kushirikiana na Russia katika kutoa uungaji mkono mkubwa kwa kila mmoja katika masuala yanayohusu maslahi yao ya msingi, Rais wa China Xi Jinping amesema kwenye mkutano na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin, uliofanyika Samarkand Alhamisi.

Rais Xi amekutana na Putin katika ukumbi wa Forumlar Majmuasi mjini Samarkand ili kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano kati ya China na Russia na masuala ya kimataifa na kikanda yenye maslahi ya pamoja.

Xi amsema, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, China na Russia zimedumisha mawasiliano ya kimkakati yenye ufanisi.

“Ushirikiano baina ya nchi mbili katika sekta mbalimbali umesonga mbele kwa kasi, huku shughuli za Mwaka za Mabadilishano ya Kimichezo zikiendelea vyema, na kuwepo kwa kasi kubwa katika ushirikiano wa maeneo yaliyo chini ya nchi husika na mawasiliano kati ya watu,” amesema.

Xi amesema, nchi hizo mbili zimedumisha uratibu wa karibu katika ngazi ya kimataifa ili kudumisha kanuni za msingi za uhusiano wa kimataifa.

Xi ameeleza kwamba, katika kukabiliana na mabadiliko ya Dunia, ya zama na historia, China itashirikiana na Russia kutimiza wajibu wao kama nchi kubwa na kuchukua nafasi kubwa katika kuleta utulivu katika ulimwengu wenye mabadiliko na kukosekana kwa utaratibu.

Amesisitiza kuwa China itashirikiana na Russia kuimarisha ushirikiano wa kivitendo katika biashara, kilimo, muunganisho na maeneo mengine.

Xi ameeleza kuwa, pande hizo mbili zinahitaji kuimarisha uratibu chini ya mifumo ya pande nyingi ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), Mkutano wa Hatua za Maingiliano na Kujenga Imani barani Asia na BRICS ili kuhimiza mshikamano na kuaminiana kati ya pande mbalimbali, kupanua ushirikiano wa vitendo, na kulinda maslahi ya usalama ya kikanda pamoja na maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea na masoko yanayoibukia.

Kwa upande wake, Putin ameutakia Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) mafanikio kamili na kusema anaamini kuwa chini ya uongozi wa Rais Xi, China itaendelea kupata mafanikio mapya katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Putin ameweka bayana kuwa Dunia inapitia mabadiliko mengi, lakini jambo pekee ambalo bado halijabadilika ni urafiki na kuaminiana kati ya Russia na China, na kwamba ushirikiano wa kimkakati wa uratibu wa pande zote kati ya Russia na China uko imara kama milima.

“Russia na China zote mbili zinalinda utaratibu wa kimataifa wenye usawa na unaokubalika zaidi, zikiweka mfano mzuri katika uhusiano wa kimataifa,” amesema.

Ameeleza kuwa upande wa Russia unaheshimu kwa dhati kanuni ya kuwepo kwa China moja na kulaani hatua za uchochezi zinazofanywa na nchi moja moja katika masuala yanayohusu maslahi ya msingi ya China.

Putin amesema Russia itaimarisha na kujenga kwa kina mawasiliano na ushirikiano kati ya pande mbili na wa pande nyingi na China, na kupanua ushirikiano katika sekta muhimu kama vile uchumi, biashara na nishati.

Amesema Russia itashirikiana na China kuhimiza ushirikiano wa kina kati ya nchi wanachama wa SCO kwa kuzingatia kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, ili kujenga jukwaa lenye mamlaka la kudumisha usalama na utulivu wa kikanda.

Rais wa China Xi Jinping akikutana na Rais wa Russia Vladimir Putin katika Ukumbi wa Forumlar Majmuasi mjini Samarkand, Uzbekistan, Septemba 15, 2022. (Xinhua/Zhai Jianlan)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha