Uganda yalaani Bunge la EU kuzuia maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi ya nchi hiyo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 16, 2022

KAMPALA - Bunge la Uganda Alhamisi wiki hii limelaani azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) la kusitisha maendeleo ya sekta ya mafuta nchini humo, likitaja wasiwasi wa mazingira na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Bunge la EU lilizishauri Uganda na Tanzania kutoendelea na ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki litakalosafirisha mafuta hayo kutoka Magharibi mwa Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania. EU pia ilizionya nchi wanachama wake kutotoa msaada wa kidiplomasia, kifedha au mwingine wowote kwa miradi ya mafuta na gesi ya Uganda.

Thomas Tayebwa, Naibu Spika wa Bunge la Uganda, amesema azimio la Bunge la EU linalenga kupunguza maendeleo ya mafuta na gesi ya Uganda na kwa kiwango kikubwa, ukuaji wa uchumi wa jamii na maendeleo ya nchi hiyo.

"Pia linalenga kuwanyima Waganda na Watu wa Afrika Mashariki faida na fursa kutoka kwenye sekta ya mafuta na gesi. Hii inawakilisha aina ya juu kabisa ya Ubaguzi wa Kiuchumi dhidi ya nchi zinazoendelea," Tayebwa amesema.

"Si busara kusema kwamba miradi ya mafuta ya Uganda itaongeza athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini ni ukweli kwamba Umoja wa Ulaya wenye asilimia 10 tu ya idadi ya watu duniani unatoa asilimia 25 ya hewa chafu duniani, na Afrika yenye asilimia 20 ya idadi ya watu wote duniani, inatoa asilimia 3 ya hewa chafu. EU na nchi nyingine za Magharibi kihistoria zinahusika na athari za mabadiliko ya tabianchi. Nani basi anapaswa kuacha au kupunguza kasi ya maendeleo ya maliasili? Hakika si Afrika au Uganda," ameongeza.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema mapato yatakayopatikana kutokana na mafuta hayo yatakuwa muhimu katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi ya nchi na kikanda.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha