Siri ya Mafanikio ya China

By Ephrahim Bahemu (Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 16, 2022

Ukizungumzia mgawanyo wa nchi duniani katika suala la maendeleo upo katika makundi mawili; yaani nchi zilizoendelea na zinazoendelea, hakuna neno rasmi kwa nchi ambazo hazijaendelea.

Ambao wanaendelea na ambao hajawajaendelea na wanazidi kumezwa na wimbi la umaskini wote wapo katika kapu moja la nchi zinazoendelea, lakini katika kapu hilo ambalo bara la Afrika limechangia idadi kubwa kuna wakubwa, tena wakubwa sana.

China ni miongoni mwa nchi zinazotajwa kuwa bado zinaendelea pamoja na mafanikio makubwa waliyofikia, lakini katika viwango vya upimaji wa maendeleo vinavyotumika sasa haipo kwenye orodha ya nchi zilizoendelea.

Hata hivyo, ni Taifa la pili kwa uchumi duniani kwa kuzingatia pato la Taifa ambalo ni Dola za Marekani trilioni 15.72, ikiwa nyuma ya Marekani ambayo pato lake ni Dola trilioni 20.89.

Kwa kuwa upimaji wa nchi iliyoendelea pamoja na mambo mengine wanaangalia pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka, pengine China, inayoongoza kwa idadi kubwa ya watu duniani inakwamia hapo, lakini bila shaka maendeleo ya Taifa kwa ujumla ni sawa au hata zaidi ya mataifa yaliyoendelea.

China, ambayo ni Taifa kubwa lenye nguvu ya kiuchumi duniani ndiyo inayoongoza katika kundi la nchi zinazoendelea, zikiwamo nyingine nyingi kutoka katika bara rafiki la nchi hiyo (Afrika).

Pamoja na kuwa katika kapu moja, ni dhahiri hakuna ufanano, pamoja na kwamba miaka ya nyuma kuna baadhi ya nchi za Afrika, ikiwemo Kenya zilikuwa na pato kubwa la Taifa kuliko China, lakini hivi sasa China iko mbali na imekuwa ni kimbilio la mataifa mengi yanayoendelea kuomba msaada na mikopo.

Mataifa mengi bado yanatamani kuiga au kujua China iliwezaje kutoka katika wimbi zito la umaskini na kuwa miongoni mwa mataifa makubwa yenye nguvu ya kiuchumi ndani ya kipindi kisichozidi miongo saba.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kutoka Afrika, Mkurugenzi katika Wizara ya mambo ya nje ya China anayeshughulikia masuala ya Afrika, Wu Peng alisema ili nchi iendelee inahitaji uongozi imara, sera za muda mrefu na usalama.

Kuhusu siri ya mafanikio ya China, anasema maendeleo yaliyopo ni matokeo ya siasa thabiti na sera endelevu, huku akiweka tahadhari kuwa muundo unaotumika nchini mwake unaweza usilete matokeo chanya kwa nchi nyingine, ila muhimu ni kuangalia kile kinachofaa kwa mazingira ya nchi husika.

“Hatusemi kuwa muundo na aina yetu ya siasa na uongozi ndiyo unafaa kwa nchi nyingine zinazoendelea, hapana, kila mmoja anaweza kutafuta njia yake kulingana na mazingira, lakini kwetu sisi muundo huu ndio unaotufaa,” anasema Peng.

Anasisitiza kuwa nchi inayotaka maendeleo ni lazima iwe na uongozi imara, siyo imara tu, bali uwe salama na muhimu zaidi ni kuwekeza kwa kizazi kijacho, kwani hivyo vitu vimeonyesha kufanya kazi katika mataifa mengi, ikiwemo China.

“Kusimamia kizazi kijacho ni muhimu sana kwa sababu ndicho kitakachokuja kuongoza nchi kwa namna moja ama nyingine.

“Taifa imara linalotaka maendeleo linapaswa kuwekeza zaidi huku, kuwa na uongozi imara na uhakika wa usalama,” anasema.

Peng anasema hivi sasa China inatilia mkazo ushirikiano wake na bara la Afrika, ambalo wamekuwa na urafiki wa muda mrefu na ana imani ushirikiano huo utaleta matokeo chanya ya kimaendeleo kwa pande zote mbili.

Anasema kwa sasa mizania ya biashara kati ya Afrika na China haipo katika usawa kwa sababu ya muundo wa kiuchumi wa nchi hizo mbili, lakini kwa sababu wao kwa sasa ni wazalishaji wakubwa duniani na bidhaa wanazozalisha zinahitajika kwa watu wengi.

Anasema China hivi sasa kupitia mpango wake wa ushirikiano na bara la Afrika unaendana na malengo ya Afrika ya mwaka 2063 ya kukuza uzalishaji na kuwa na uhakika wa kujitegemea katika masuala muhimu.

“Afrika kuna ardhi kubwa na nzuri, lakini bado mnategemea nafaka kutoka nje ya nchi, kinachohitajika ni sera nzuri tu ya kukuza sekta ya kilimo na uzalishaji ili hata inapotokea changamoto popote duniani msiathirike katika usalama wa chakula, lakini vilevile mtakuza biashara kimataifa,” anasema Peng.

Akizungumzia suala la mikopo kwa mataifa ya Afrika, alisema sio nchi za Afrika tu, nchi zote duniani, ikiwemo China inahitaji mikopo kwa ajili ya maendeleo .

“Kuhitaji mikopo sawa, kikubwa ni kuangalia aina ya mkopo na kuusimamia vizuri ili malengo yafikiwe. Lakini pia kupanga kulingana na uwezo,” anasema Peng.

Kuhusu sera za kidunia za kulinda mazingira na kupambana na ongezeko la joto duniani, Peng anasema China inafikiri kupunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya nishati chafu kwa miaka michache ijayo.

Anasema kwa mataifa mengine yanayoendelea, hususan ya Afrika yanapaswa kufikiria jambo hilo kwa kina.

Anafafanua mataifa yanayoendelea bado yanahitaji kiwango kikubwa cha nishati na ni vigumu kwao kumudu nishati jadidifu.

“Mataifa hayo hayalazimishwi kuwa na mpango wa kupunguza hewa ya ukaa kwa kuwa bado yanapambana kuendelea, hilo lisiwafumbe macho, wafikirie kupunguza hewa hiyo kadiri wanavyoweza,” anasema.

Kuhusu ushirikiano wa kiusalama, anasema nchi hiyo inasaidia pale watu wa Taifa husika wanapokuwa wanahitaji msaada, pia hushiriki katika vikosi vya ulinzi wa amani vya Umoja wa Mataifa, ingawa ikitokea wananchi hawataki China itaviondoa.

(kutoka MWANANCHI )

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha