CPC: China imeweka kipaumbele maisha ya watu

By Ephrahim Bahemu (Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 19, 2022

Beijing. Wakati kukiwa na ukosoaji mwingi duniani kuhusu sera ya China ya kupambana na ugonjwa wa Uviko-19 maarufu ‘zero covid policy’, Chama tawala nchini humo kimeitetea kikisema imekuwa msaada mkubwa kwa nchi.

Kumekuwa na ukosoaji wa sera hiyo kutoka kwa watu mbalimbali hususani wa mataifa ya magharibi wakisema sera hiyo ina viashiria vya China kujitenga na dunia lakini leo Jumamosi Oktoba 15, 2022, msemaji wa Chama cha Kimomunisti cha China (CPC), Sun Yeli amesema nchi hiyo imeweka kipaumbele maisha ya watu.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka mataifa mbalimbali waliopo jijini Beijing kuhudhuria kongamano la kitaifa la 20 la CPC linalotarajiwa kuanza leo, Kangamnao hilo pamoja na mambo mengine ndilo litakuja na majibu iwapo Rais wa sasa Xi Jinping ataendelea kwa muhula wa watatu au kutakuwa na Rais mpya.

“Sera ya ‘zero Covid’ inatokana na uhalisia uliopo ndani ya China na inazingatia njia za kisayansi za kukabiliana na ugonjwa huo, tunapambana kuhakikisha maisha ya kawaida yanarejea na sera hii inatusaidia kupunguza kasi ya kuenenea kwa ugonjwa huo,” amesema Yeli.

Amesema Uviko-19 umeathiri uchumi na maisha ya watu duniani kote na kila mtu anatamani kuona dunia inatokomeza ugonjwa huo na kurejea katika maisha ya kawaida.

Itakumbukwa Ugonjwa wa Uviko-19 uliripotiwa kwa mara ya kwanza Desemba, 2019 katika jimbo la Wuhan nchini China, tangu wakati huo hatua nyingi zimechukuliwa dunia kote kukabiliana na ugonjwa huo lakini baada ya kupatikana kwa chanjo masharti mengi yalilegezwa.

Kwa sasa China ndiyo nchi ambayo imesalia na madhubuti ya kukabiliana na ugonjwa huo, mbali na kuchanja watu wake nchini china, bando kunapotokea visa vipya watu hufungiwa katika makazi yao lakini vilevile ili kuingia katika sehemu mbalimbali za huduma nchini China ni lazima uwe umepima walau siku tatu zilizopita na hujakutwa na maambukizi.

Kuhusiana na suala la uchumi China ambayo imefanikiwa kukuza pato lake la taifa mara mbili zaidi ndani ya kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Rais Xi Jinping, inasema kulingana na ukweli kuwa hivi sasa uchumi wake ni mkubwa ni vigumu kwa wao kuendelea kuwa ukuaji wa uchumi kwa kasi ileile.

“Kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita kasi ya ukuaji wetu wa uchumi ilikuwa kwa wastani wa asilimia 6.6 na tulichangia asilimia 30 ya ukuaji wa pato la dunia katika kipindi husika, ni vigumu kuendelea kuwa na ukuaji huo kulingana na ukubwa wa uchumi, msisitizo sasa ni uendelevu,” amesema.

Amesema taifa hilo limekuwa na ukuaji mzuri wa uchumi na wa uhakika na licha mlipuko wa Uviko-19, uchumi wa China ulifanya vizuri miongoni mwa mataifa mengine, “Misingi yetu ya kukuza uchumi imara bado haijabadilika misisitizo sasa ni uchumi endelevu na usalama katika Nyanja zote”

Hivi sasa ni ya pili kwa uchumi duniani ikiwa nyuma ya Marekani, pato linalofikia Trilioni 15.72 hadi mwaka 2021 na huwenda kiwango hicho kikaongezeka zaidi mwaka huu kwani katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka lilifika dola trilioni 8.86. Tanzania pato letu la Taifa ni dola bilioni 68.8 mwaka 2021.

Mwaka 2012 wakati Rai Xi Jinping anaingia madarakani pato la Taifa la China lilikuwa Dola Trilioni 8.5.

(kutoka MWANANCHI)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha