Rais wa Tanzania ahamasisha matumizi ya nishati safi kupikia chakula

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 02, 2022

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kwenye jukwaa) akizungumza kwenye Kongamano la kwanza la Matumizi ya Nishati safi ya kupikia jijini Dar es Salaam, Tanzania, Novemba 1, 2022. Rais Samia Jumanne ameagiza mamlaka za serikali kuunda kikosi kazi cha taifa cha wataalam kitakachotengeneza mpango mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kupikia. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)

DAR ES SALAAM, - Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Jumanne ameagiza mamlaka za serikali kuunda kikosi kazi cha taifa cha wataalam kitakachotengeneza mpango mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kupikia.

Rais Samia amesema kikosi kazi cha Taifa kitakachoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuratibiwa na Wizara ya Nishati kitasaidia kukomesha matumizi ya mkaa na kuni kwa kupikia hali inayosababisha uharibifu wa mazingira na madhara ya kiafya.

Akifungua Kongamano la kwanza la Matumizi ya Nishati safi kupikia chakula jijini Dar es Salaam, Tanzania, Samia amesema kikosi kazi hicho kitapewa jukumu la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia katika miaka kumi ijayo.

Kongamano hilo la siku mbili linalenga kupata uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau kuhusu hali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania na kubadilishana uelewa na uzoefu katika kukabiliana na changamoto ya kutumia biomasi kupikia.

“Misitu inaangamizwa kwa kasi kubwa katika mikoa ya Morogoro, Lindi na Ruvuma kwa kutengeneza mkaa na kuni, hili lazima likome,” amesema Rais Samia.

Amesema serikali ya awamu yake, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, itatenga bajeti kwa ajili ya kuanzisha mfuko unaolenga kusaidia utafiti, teknolojia na ubunifu wa kupika kwa nishati safi.

Samia ameiagiza Wizara ya Nishati ya Tanzania kuhakikisha taasisi zenye watu zaidi ya 300 zikiwemo shule, hospitali na magereza zinaacha matumizi ya mkaa kwa kupikia na badala yake kutumia nishati safi ikiwamo gesi asilia ya kimiminika.

Waziri wa Nishati wa Tanzania January Makamba amesema mkutano huo utatumika kama jukwaa la mazungumzo ili kuwezesha nchi hiyo kuelekea katika matumizi ya nishati safi.

“Serikali ya Tanzania imedhamiria kuboresha maisha ya watanzania kwa kupunguza na hatimaye kuondoa madhara ya kiafya, kimazingira na kijamii yatokanayo na upishi unaotumia biomasi,” amesema Makamba.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha