Mwandishi wa Habari Rashid Kejo: China imetimiza ahadi zake kwa vitendo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 02, 2022

Rashid Kejo kwenye Jumba Kuu la Mikutano ya Umma la China wakati wa Mkutano Mkuu wa 19 wa Chama cha Kikomunisti cha China. (Picha ilitolewa na mhojiwa.)

Beijing -- Hivi karibuni Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) uliovutia ufuatiliaji kutoka nchi mbalimbali umefungwa hapa Beijing,.

Mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi la Tanzania Rashid Kejo ni mmoja wa waandishi wengi wa habari waliokuja mpaka Beijing kuripoti Mkutano Mkuu wa 19 wa CPC mwaka 2017. Ingawa mwaka huu hajatembelea jumba la kufanyia mkutano, amefuatilia mkutano huo kwa mbali. Amesema, China imetimiza ahadi zake kwa vitendo.

Bw. Kejo bado anakumbuka vizuri safari yake ya kuja Beijing miaka mitano iliyopita. Anasema, kuripoti mkutano mkuu wa 19 wa CPC kumempa fursa ya kufuatilia mambo yanayoendelea katika chama hicho, hasa mwaka huu ambapo umefanyika uchaguzi mwingine.

Katika mahojiano yake na People’s Daily online Swahili, Bw. Kejo amesifu mafanikio ya China ya kuhakikisha wanavijiji wote walioishi chini ya mstari wa umaskini wanaondokana na umaskini, ambayo yalitajwa kwenye ripoti ya Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC. Bw.Kejo amesema, “Mkakati wake unajali watu wa mashinani. Ulikuwa mpango wenye uhalisia na uliolenga kuleta maisha bora kwa watu wote.”

“Naamini kwamba vita kubwa ambayo dunia inapigana nayo ni kuondoa umaskini, na ikiwa Tanzania itapata fursa ya kujifunza mafanikio haya itapiga hatua kubwa na ya kupigiwa mfano siyo kwa nchi jirani tu, bali nchi zote zinazoendelea,” amesema Kejo.

Chama cha Kikomunisti cha China kimeanzisha majukwaa mengi ya mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya vyama vya siasa vya dunia nzima, ili kujadiliana na vyama mbalimbali kuhusu wajibu wa kuwapatia watu furaha. Kejo anakubaliana sana na maoni hayo. Ameisifu Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichoanzishwa mwezi wa Februari mwaka huu nchini Tanzania, ambacho ni moja ya majukwaa ya mawasiliano kati ya vyama kutoka nchi sita za Kusini mwa Afrika na CPC kimeshirki kwenye ujenzi wake.

“Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere siyo tu itasaidia ujenzi wa vyama kwa nchi hizo sita kwa Afrika, bali kitawajengea uwezo wa vijana wa vyama husika wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia kwa sasa ambayo inahitaji maarifa makubwa na mbinu za kisasa,” amesema Bw. Kejo.

Kejo pia amefuatilia zaidi mambo kuhusu ushirikiano wa kimataifa kwenye ripoti iliyotolewa katika mkutano huo, ambayo ilitaja kuwa, China itashikilia kithabiti sera ya kimsingi ya kufungua mlango, na mkakati wa uwazi wa kufanya ushirikiano wa kunufaishana, ili kutoa fursa mpya kwa dunia kupitia maendeleo ya China.

Bw. Kejo amesema, China ni rafiki mkubwa wa Tanzania. Miradi mingi iliyojengwa chini ya ushirkiano wa nchi hizo mbili ni ya kimkakati na inawasaidia wananchi walio wengi. “Daraja la Magufuli kwa mfano, likikamilika litakuwa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki likiwa na urefu wa kilomita 3.2. Hili ni jambo kubwa sana kwa Watanzania.”

“China imetimiza ahadi zake kwa vitendo. Ningependa kuona zaidi ushiriki wa China katika kusaidia maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za Afrika, hasa katika maeneo ya teknolojia rahisi kwa wananchi waishio vijijini au maeneo ya mbali,” amesema Bw. Kejo. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha