Rais Xi Jinping atuma barua ya pongezi kwa Mkutano wa Kimataifa wa Mtandao wa Intaneti wa Wuzhen wa Mwaka 2022

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 10, 2022

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping Jumatano ametuma barua ya pongezi kwa Mkutano wa Kimataifa wa Mtandao wa Intaneti wa Wuzhen wa Mwaka 2022, ambao umefunguliwa huko Wuzhen, Mkoa wa Zhejiang, Mashariki mwa China.

Katika barua hiyo, Xi ameweka bayana kuwa teknolojia ya kidijitali inazidi kuunganishwa katika sekta zote na mchakato mzima wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kuleta mabadiliko makubwa katika mitazamo ya watu ya kufanya kazi, maisha ya kila siku, na utawala wa kijamii.

Xi ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, inayokabiliwa na fursa na changamoto zinazoletwa na mfumo wa kidijitali, kujenga kwa pamoja eneo la mtandao ambalo ni lenye haki zaidi na usawa zaidi, lililo wazi zaidi na linalojumuisha watu wote, salama na thabiti zaidi, na lenye nguvu zaidi.

“China iko tayari kushirikiana na nchi mbalimbali duniani ili kuanzisha njia ya kimataifa ya maendeleo ya kidijitali inayofanya ushirikiano wa kidijitali katika kujenga na kunufaika pamoja rasilimali za kidijitali, uchumi unaostawi wa kidijitali, usimamizi wenye ufanisi mkubwa wa kidijitali, utamaduni unaostawi wa kidijitali, usalama wa kidijitali unaohakikishwa ipasavyo, na ushirikiano wa kunufaishana ili kupata maendeleo kwa pamoja ” Rais Xi amesema.

Ameongeza kuwa, jitihada za haraka zinapaswa kufanywa ili kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja katika nafasi ya mtandao, kuchangia hekima na nguvu kwa amani na maendeleo ya Dunia pamoja na maendeleo ya ustaarabu wa binadamu.

Mkutano huo umefunguliwa Jumatano ukiwa na kaulimbiu isemayo "Kuelekea Mustakabali wa Pamoja wa Kidijitali katika Ulimwengu Uliounganishwa -- Kujenga Jumuiya yenye Mustakabali wa Pamoja katika nafasi ya Mtandao."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha