Rais Xi Jinping atoa hotuba ya maandishi kwenye Jukwaa la Kimataifa la Msaada wa Mpunga Chotara na Usalama wa Chakula Duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 14, 2022

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ametoa hotuba ya maandishi kwenye Jukwaa la Kimataifa la Msaada wa Mpunga Chotara na Usalama wa Chakula Duniani, ambalo limefanyika Jumamosi mjini Beijing.

Katika hotuba yake, Xi ameweka bayana kuwa usalama wa chakula ni msingi kwa maisha ya binadamu. Na kwamba, nusu karne iliyopita, upandaji wa mpunga chotara uliendelezwa kwa mafanikio na kupandwa kwa wingi nchini China. Amesema, kutokana na teknolojia hiyo, China imeweza kulisha karibu asilimia 20 ya watu wote duniani chini ya asilimia 9 ya ardhi inayolimwa duniani, na imekuwa nchi inayozalisha chakula kwa wingi na ya tatu kwa kuuza chakula duniani.

“Kuanzia Mwaka 1979, mpunga chotara ulianza kutambulishwa duniani, na kuleta manufaa kwa karibu nchi 70 katika mabara matano. Huu umekuwa mchango wa ajabu katika ongezeko la pato la nafaka la nchi hizo na maendeleo ya kilimo, na kutoa suluhisho la China kwa uhaba wa chakula katika nchi zinazoendelea,” Xi amesema.

Amesema, kwa sasa, usalama wa chakula duniani unakabiliwa na changamoto na matatizo magumu. Na kwamba, China itaendelea kushirikiana na nchi zote kwa moyo wa mshikamano na mustakabali wa pamoja ili kuendeleza Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, kuongeza ushirikiano katika usalama wa chakula na kupunguza umaskini, na kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa haraka wa Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 na kujenga Dunia isiyo na njaa na umaskini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi alishiriki kwenye shughuli hiyo, ambapo alisoma hotuba hiyo ya maandishi ya Rais Xi.

Wang amesema, Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China uliomalizika hivi karibuni ulitangaza kuwa China itatoa mchango mpya kwenye maendeleo ya binadamu kwa maendeleo ya kisasa ya China na kutoa fursa mpya kwa Dunia kwa maendeleo mapya ya China.

“Teknolojia ya upandaji wa mpunga chotara ni kumbukumbu katika historia ya sayansi na teknolojia ya kilimo nchini China, ambayo siyo tu kwamba inasaidia China kufikia muujiza wa kujitosheleza kwa chakula, lakini pia inatoa mchango muhimu katika kutatua uhaba wa chakula duniani,” Wang ameeleza.

Wang amesema China imefanya usalama wa chakula kuwa moja ya maeneo ya kipaumbele katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Dunia na kuongeza kuwa China iko tayari kufanya juhudi za pamoja na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa ili kutoa mchango mpya na mkubwa zaidi katika kulinda usalama wa chakula duniani na kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030.

Shughuli hiyo iliandaliwa kwa pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa la China, Wizara ya Kilimo na Vijiji ya China, na Idara ya Taifa ya Chakula na Akiba za Kimkakati ya China.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi akisoma hotuba ya maandishi ya Rais Xi Jinping wa China wakati akishiriki kwenye Jukwaa la Kimataifa la Msaada wa Mpunga Chotara na Usalama wa Chakula Duniani, Novemba 12, 2022. (Xinhua/Wang Ye)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha