Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping atoa wito wa kukabiliana na changamoto za nyakati pamoja kwenye mkutano wa kilele wa G20
Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba yenye kichwa kisemacho "Kushirikiana Pamoja Kukabili Changamoto za Nyakati Zetu na Kujenga Mustakabali Bora" katika Mkutano wa 17 wa kilele wa Kundi la 20 (G20) wa Bali, Indonesia, Novemba 15, 2022. Mkutano wa G20 umeanza jana hapa Jumanne. (Xinhua/Ju Peng)
BALI, Indonesia - Rais wa China Xi Jinping amehutubia Jumanne kwenye mkutano wa kilele wa Kundi la 20 (G20) wa Bali, akisema kuwa zikiwa zinakabiliwa na changamoto, nchi zote zinapaswa kuwa na uelewa juu ya jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja, na kutetea amani, maendeleo, na ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote.
Katika hotuba yake yenye kichwa kisemacho "Kushirikiana Pamoja Kukabili Changamoto za Nyakati Zetu na Kujenga Siku za Baadaye" Xi amesema Dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa ambayo hayajapata kuonekana katika miaka mia moja iliyopita, ambayo yana athari kwa Dunia, nyakati zetu na historia.
Amesema kuwa janga la virusi vya korona bado linaendelea huku maambukizi mapya yakiongezeka hapa na pale; uchumi wa Dunia unazidi kuwa tete; mazingira ya siasa za kijiografia yana hali ya wasiwasi; usimamizi wa kimataifa bado unakosekana; matatizo ya chakula na nishati yanachanganyikana. "Haya yote yanaleta changamoto kubwa kwa maendeleo ya binadamu," Xi ameweka bayana.
Amesema nchi zote zinapaswa kushikamana pamoja kujibu swali la nyakati -- "nini hakiko sawa kwa Dunia hii, nini tunapaswa kufanya juu yake" -- ili kukabiliana na matatizo na kujenga pamoja maisha bora ya baadaye.
Huku akitoa wito kwa nchi zote kuheshimiana, kutafuta misingi ya pamoja huku zikihifadhi tofauti, kuishi pamoja kwa amani, na kukuza uchumi wa dunia ulio wazi. Hakuna nchi inayopaswa kutafuta maslahi ya upande mmoja, 'kujenga kuta ndefu kwenye ua mdogo', na kutenganisha wengine kwa kufanya ushirikiano wa pande chache.
Rais Xi amesema, nchi zote za G20, wanapaswa kuchukua jukumu la asili la kuwa washiriki wakuu wa kimataifa na kikanda, na wanapaswa kuongoza kwa mfano katika kuhimiza maendeleo ya mataifa yote, kuboresha ustawi wa wanadamu wote, na kusukuma mbele maendeleo ya Dunia nzima.
"Huku ustaarabu wa binadamu ukiwa tayari katika karne ya 21, mawazo ya Vita Baridi kwa muda mrefu yamepitwa na wakati. Tunachohitaji kufanya ni kushikana mikono na kuinua ushirikiano wetu wa kunufaishana ili kufikia kiwango kipya," amesema.
Huku akitaka nchi zilizoendelea kuzishika mkono zile ambazo zinaendelea, Xi amesisitiza haja ya kufanya maendeleo ya kimataifa kuwa yenye manufaa kwa wote, akisema kuwa maendeleo ni ya kweli tu pale nchi zote zinaendelea pamoja.
China imependekeza Mpango wa Maendeleo ya Dunia (GDI), na kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kusini na Kusini, Xi amesema, huku akiongeza kuwa China itaongeza ufadhili kwa Mfuko wa Amani na Maendeleo wa China na Umoja wa Mataifa, na inashirikiana na nchi na mashirika ya kimataifa zaidi ya 100 kuhusu GDI, hivyo kutoa msukumo mpya wa utekelezaji wa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.
Xi amezitaka pande zote kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa dhidi ya maambukizi ya virusi vya korona , kupunguza mfumuko wa bei duniani, na kupunguza hatari za kimfumo za kiuchumi na kifedha, huku akiongeza kuwa nchi zenye uchumi ulioendelea lazima zikabiliane na athari za marekebisho ya sera za kifedha ili zisiathiri Dunia nzima.
"Taasisi za fedha za kimataifa na wakopeshaji wa kibiashara ambao ndiyo wakopeshaji wakuu wa nchi zinazoendelea wanapaswa kushiriki katika kupunguza na kusimamisha madeni kwa nchi zinazoendelea," amesema na kuongeza kuwa China inatekeleza Mpango wa G20 wa kuahirisha muda wa malipo ya kulipa madeni kwa nchi husika.
"Tunapaswa kuendelea kushikilia mfumo wa biashara wa pande nyingi unaozingatia WTO, kusukuma mbele mageuzi ya WTO, kuimarisha biashara huria na kuwezesha uwekezaji," amesema.
Xi pia amesisitiza haja ya kufanya juhudi kubwa katika kukabiliana na mfumuko wa bei na mgogoro wa nishati ili kuhakikisha uchumi wa Dunia unabaki kwenye viwango vinavyofaa vya ukuaji.
Rais Xi Jinping wa China akielekea kwenye eneo la mkutano wa 17 wa kilele wa Kundi la 20 (G20) huko Bali, Indonesia, Novemba 15, 2022. (Xinhua/Ju Peng)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma