Rais Xi Jinping asema China kuendelea kushirikiana na wanachama wa G20 kuhusu uchumi wa kidijitali duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 17, 2022

Rais Xi Jinping wa China akihudhuria na kuhutubia mkutano wa 17 wa kilele wa Kundi la 20 (G20) kisiwani Bali, Indonesia, Novemba 16, 2022. (Zabur Karuru/Kituo cha Vyombo vya habari cha G20 Indonesia/Kutumwa kwa Xinhua)

BALI, Indonesia - China itaendelea kushirikiana na wanachama wa Kundi la 20 (G20) ili kuhimiza dhana ya uchumi wa kidijitali wa kimataifa wenye uwiano, ulioratibiwa na jumuishi ambao unaleta manufaa kwa wote na unaoonyesha ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote na mafanikio ya pamoja, Rais Xi Jinping wa China amesema Jumatano.

Xi ameyasema hayo wakati alipohudhuria na kuhutubia mkutano wa 17 wa G20 katika kisiwa cha mapumziko cha Bali, Indonesia.

Kwenye majadiliano juu ya mabadiliko ya kidijitali, Xi alisema kuwa ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kasi ya mabadiliko ya kidijitali kote duniani yamekuwa mambo muhimu yanayoathiri hali ya uchumi wa Dunia.

Amesema, China ilipokuwa mwenyeji wa Mkutano wa G20 wa Hangzhou Mwaka 2016, ilijumuisha uchumi wa kidijitali katika ajenda za G20 kwa mara ya kwanza, na kutoa wito wa kutafuta njia ya maendeleo kutegemea uvumbuzi na kutafuta vichochezi vipya vya ukuaji wa uchumi.

Katika miaka ya hivi karibuni, G20 imejenga maelewano zaidi na kuongeza ushirikiano katika kukabiliana na mabadiliko ya kidijitali na kujenga uchumi wa kidijitali, amesema, huku akielezea matumaini yake kwamba pande zote zitaibua nguvu katika ushirikiano wa kidijitali na kuleta manufaa ya uchumi wa kidijitali kwa watu wa nchi zote.

Ametoa wito kwa nchi kushikilia msimamo wa pande nyingi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

“Nchi mbalimbali zinapaswa kufanya juhudi za pamoja ili kuhimiza mazingira yenye uwazi, jumuishi, usawa, haki na yasiyo ya ubaguzi kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali, na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kukuza tasnia ya kidijitali na kukuza mageuzi ya kidijitali ya viwanda, ili kuibua uwezo wa uchumi wa kidijitali katika kuhimiza ukuaji wa uchumi wa kimataifa,” Rais wa China amesema.

Kujenga "ua mdogo wenye uzio mrefu" ili kupunguza au kuzuia ushirikiano katika sayansi na teknolojia kutaumiza maslahi ya wengine bila kujinufaisha, Xi ameeleza huku akiongeza kuwa vitendo hivyo haviendani na maslahi ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa.

Xi amesema ni muhimu kuyapa kipaumbele maendeleo na kuziba pengo la kidijitali, akisema nchi zinapaswa kwa pamoja kuhimiza muunganisho katika zama ya kidijitali, na kuchukua hatua madhubuti za kukuza uelewa na ujuzi wa kidijitali kwa wote.

“Ni muhimu sana kusaidia nchi zinazoendelea na makundi yaliyokosa fursa kukabiliana na mabadiliko ya kidijitali na kujitahidi kupunguza pengo la kidijitali,” amesisitiza.

China imezindua mpango wa kujenga njia ya kidijitali ya Hariri, na imeuweka uchumi wa kidijitali kuwa eneo muhimu la ushirikiano chini ya Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Xi amesema, huku akiweka wazi kuwa China inatarajia kushirikiana na pande zote katika suala hili.

Xi pia ametoa wito wa kufanyika kwa juhudi za kimataifa katika kufuata mbinu inayoendeshwa na uvumbuzi na kuwezesha kufufuka kwa uchumi baada ya janga la UVIKO-19.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha