NATO na Poland zasema mlipuko wa kombora katika kijiji cha Poland haukuwa shambulio la Russia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 17, 2022

BRUSSELS/WARSAW - Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO), amesema mjini Brussels Jumatano kwamba mlipuko katika Kijiji cha Przewodow cha Poland karibu na mpaka na Ukraine Jumanne usiku huenda halikuwa shambulizi kutoka kwa Russia bali ulisababishwa na kombora la ulinzi wa anga la Ukraine. Watu wawili waliuawa katika mlipuko huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Warszawa kufuatia mkutano wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Poland siku ya Jumatano, Rais wa Poland Andrzej Duda ameunga mkono kauli ya Stoltenberg na kusema kuwa "Hatuna uthibitisho katika hatua hii kwamba ni kombora lililorushwa na Russia. Kuna dalili nyingi kwamba lilikuwa ni kombora la ulinzi wa anga ambalo kwa bahati mbaya lilianguka kwenye eneo la Poland." Amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba kombora hilo lilikuwa roketi ya S-300 iliyotengenezwa Russia, ambayo huenda ilitengenezwa miaka ya 1970.

"Hakuna kitu, hakuna chochote cha kuthibitisha kwamba lilikuwa shambulio la kukusudia dhidi ya Poland. Kilichotokea -- kwamba roketi ilitua kwenye eneo letu -- haikuwa kwa makusudi ... Haikuwa shambulio dhidi ya Poland," Duda amesema.

Huku akirejea matokeo ya uchunguzi wa awali wa vifusi vilivyopatikana katika eneo la mlipuko, Stoltenberg amesema baada ya mkutano wa dharura wa NATO katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels kuhusu suala hili kwamba "Hatuna kiashilio kwamba hii ilikuwa matokeo ya shambulio la makusudi. Na hatuna kiashilio kwamba Russia inaandaa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya NATO."

Amesema "Tukio hilo, huenda lilisababishwa na kombora la ulinzi wa anga la Ukraine lililofyatuliwa kulinda eneo la Ukraine dhidi ya mashambulizi ya makombora kutoka upande wa Russia."

Stoltenberg na Duda wote wamesema uchunguzi unaendelea. Stoltenberg ametoa wito wa kuwa na subira na akaonya dhidi ya kukurupuka kufikia hitimisho -- msimamo ambao pia unaoungwa mkono na washirika wote wa NATO.

“Nilizungumza na Rais Duda jana usiku, tulikubaliana umuhimu wa kusubiri matokeo ya uchunguzi, hatuna matokeo ya mwisho ya uchunguzi unaoendelea,” Amesema.

Amesisitiza haja ya kuzuia kuchochea mgogoro.

Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki alisema kuwa huenda isiwe muhimu kutumia Kifungu cha 4 cha Mkataba wa NATO.

Kifungu cha 4 kinasema kwamba "Pande zitashauriana wakati wowote, kwa maoni ya yeyote kati yao, ikiwa ukamilifu wa ardhi, uhuru wa kisiasa, au usalama wa mshirika yeyote utatishiwa."

Hata hivyo, Poland imeweka baadhi ya vitengo vya kijeshi katika hali ya juu ya utayari.

Mjini Moscow, Wizara ya Ulinzi ya Russia imekanusha ripoti kwamba makombora ya Russia yamepiga eneo la Poland, na kuyataja madai hayo kama "uchochezi wa makusudi unaolenga kuzidisha hali hiyo." 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha