Maadili ya kazi ya Wachina yampa furaha mfanyakazi wa TAZARA mwenye umri wa miaka 70

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 18, 2022

John Mulenga, aliyekuwa mwajiriwa wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA), akiwa katika picha huko Ndola, Jimbo la Copperbelt, Zambia, Novemba 3, 2022. (Picha na Lillian Banda/Xinhua)

LUSAKA - Hadithi ya ujenzi wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) mara nyingi imekuwa ukumbusho wa uhusiano wa muda mrefu kati ya Zambia na China.

Kwa John Mulenga, raia wa Zambia mwenye umri wa miaka 70, hadithi hiyo inazua kumbukumbu nzuri tangu Mwaka 1972 wakati yeye, akiwa kijana, alisafiri kutoka Wilaya ya Ndola Jimbo la Copperbelt hadi Wilaya ya Mpika katika Jimbo la Muchinga kutafuta ajira.

"Nilifanikiwa kupata kazi ya ukarani wa mshahara katika kampuni ya China ambayo ilipewa jukumu la kujenga reli Mwaka 1972. Nilikuwa kijana wa miaka 19 wakati huo," Mulenga ameeleza.

Anasema kuwa ni katika kipindi hiki ambapo alipata ujuzi na utaalamu katika usimamizi wa reli, ambao huutoa na kuutumia kwa urahisi kila anapoitwa.

"Nina uwezo wa kueleza masuala ya usimamizi wa reli vizuri kabisa. Na kwa sababu hiyo, baadhi ya watu wanadhani nilipata utajiri huu wa maarifa nje ya nchi. Ukweli ni kwamba sijafika hata chuo kikuu au chuo cha ufundi. Wasimamizi wangu wa Kichina walihakikisha kuwa nimepokea mafunzo yenye misingi mizuri kazini," anasema.

Akizungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua mjini Ndola, mji alikozaliwa, Mulenga anakiri mafanikio yake ya kazi yanatoka kwa wasimamizi wake wa China, ambao alisema walimpa yeye na wenzake mafunzo ya vitendo na muhimu.

 "Wachina ni walimu wazuri wanaotoa nidhamu na bidii. Sisi tuliokuwa na wasimamizi wa China tulijitokeza vizuri na mara nyingi tulikuwa tunatafutwa na waajiri," anasema.

"Nikiwa na TAZARA, nilianza kama kondakta wa treni ya abiria Februari 1976 na kupanda ngazi. Nilistaafu kama ofisa mkuu wa huduma za abiria Mwaka 2007," amesema.

Miongoni mwa mafanikio makubwa ya Mulenga hadi sasa ni mchango wake katika kuandaa kitabu cha mwongozo kwa wafanyakazi wapya wa TAZARA wa idara za biashara. Pia ameandika idadi kadhaa za makala kuhusu usimamizi wa reli.

 “Ni maarifa yale yale ambayo wasimamizi wangu wa China walinipitishia ndiyo yameniwezesha kufanya mambo haya yote ya ajabu,” amedokeza.

 Mulenga anawasihi vijana wa Zambia, ambao wana fursa ya kufanya kazi pamoja na raia wa China, kujifunza zaidi kuhusu utamaduni wa kazi wa China, ambao unawahimiza watu kufuata malengo ya muda mrefu.

 "Wachina ni wazuri katika kugawana maarifa. Mara nyingi wako tayari kuwafundisha wengine kile wanachojua. Hata hivyo, mtu anapaswa kuwa mnyenyekevu na tayari kujifunza," amebainisha.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha