Mabwawa yaliyojengwa na Wachina yaleta maji safi katika eneo lililokumbwa na ukame nchini Kenya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 21, 2022

Watoto wakinawa mikono kabla ya mlo katika shule ya chekechea huko Kimuka, Kenya, Novemba 10, 2022. (Xinhua/Dong Jianghui)

NAIROBI - Virginia Tarasha amesimama kwenye bustani yake ya mboga akimwagilia mimea yake na anatarajia mavuno mengi katika miezi michache ijayo licha ya ukame mkali ambao umeathiri sehemu nyingi za Kenya.

Mama huyo wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 48 ana kipande cha ardhi cha nusu ekari katika eneo la Kimuka, ambalo liko umbali wa takriban kilomita 40 Kusini Magharibi mwa Nairobi, mji mkuu wa Kenya, na limefunikwa na majani mabichi yenye afya licha ya jua kali katika mazingira hayo.

Tarasha ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi majuzi kwamba bahati yake ilibadilika na kuwa bora alipoanza kuchota maji ya bure kutoka kwenye mradi wa usambazaji maji wa Kimuka-Oloishoibor ambao ulizinduliwa Mwaka 2019 na uko umbali wa kilomita chache kutoka nyumbani kwake.

 "Sasa ninapata maji ambayo yanatosha kumwagilia bustani yangu kwa mwaka mzima bila kujali kama mvua inanyesha au la," Tarasha anasema.

Anaongeza kuwa kabla ya mradi huo kufika katika eneo lake, alilazimika kutembea kwa angalau saa mbili kila siku akiwa na chombo cha maji kutafuta “bidhaa hiyo” na kilimo hakikuwa cha mavuno mazuri kutokana na mvua kutonyesha.

Tarasha anasema kuwa kwa sasa shamba lake la mbogamboga nyumbani kwake linamuingizia kipato cha kutosha kumwezesha kumudu mahitaji yake ya kila siku.

 "Pia nina maji safi yanayotiririka hadi nyumbani kwangu tangu nilipounganishwa na mradi wa maji kupitia mabomba," ameongeza.

Mradi huo wa maji ulianza kutekelezwa baada ya Shirika la Barabara na Madaraja la China (CRBC) lililokuwa linajenga Reli ya Kisasa ya SGR ya kati ya Nairobi-Suswa kugundua chemichemi ya maji chini ya ardhi wakati wakichimba handaki la Ngong lenye urefu wa kilomita 4.5.

Ili kuwanufaisha wakazi wa eneo hilo, CRBC ilijenga hifadhi mbili za maji chini ya ardhi, kila moja ikiwa na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 800 ambazo huhifadhi maji hayo kabla ya kusambazwa kwa jamii bila gharama yoyote kwa watumiaji.

Chemichemi ya maji na mabwawa kwa sasa yanatunzwa na AfriStar ambayo ndiyo waendeshaji wa huduma za usafiri na mizigo za SGR.

Obed Kirwa, Msimamizi wa Kiufundi wa Njia za Reli katika Karakana ya AfriStar ya Nairobi-Maai Mahiu, amesema kuwa tangu mradi wa maji uanzishwe, eneo ambalo lilikuwa limekauka sasa ni mzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo na mifugo.

Kirwa ameongeza kuwa takriban kaya 5,000 na mifugo 10,000 kwa sasa inanufaika na mradi huo wa maji.

Amebainisha kuwa eneo hilo kwa kiasi kikubwa limeepukana na athari mbaya za ukame unaoendelea kutokana na uwepo wa vyanzo vingi vya maji.

Mkulima akiwa amesimama mbele ya tanki la kuhifadhia maji nyumbani kwake Kimuka, Kenya, Novemba 10, 2022. (Xinhua/Dong Jianghui)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha