Mwanaanga wa China Chen Dong aweka rekodi ya China ya kukaa kwenye anga ya juu kwa muda mrefu zaidi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 23, 2022

Picha ya skrini iliyopigwa katika Kituo cha Udhibiti wa Anga ya Juu cha Beijing Julai 25, 2022 ikionyesha mwanaanga wa chombo cha Shenzhou-14, Chen Dong akiwa kwenye moduli ya maabara ya anga ya juu ya Wentian. (Xinhua/Guo Zhongzheng)

BEIJING – Mwanaanga wa China Chen Dong ameweka rekodi mpya ya kukaa na kufanya kazi kwa siku nyingi zaidi kwenye anga ya juu kwa wanaanga wa China.

Shirika la Anga ya Juu la China limesema Jumanne kwamba Chen Dong ambaye ni msafiri wa anga ya juu kwa mara mbili, na ambaye yuko kwenye kituo cha anga ya juu kinachozunguka cha Tiangong cha China, amekuwa ni mwanaanga wa kwanza wa China kukaa kwenye obiti kwa zaidi ya siku 200.

Pamoja na wanaanga wengine wawili, Liu Yang na Cai Xuzhe, Chen alitumwa kwenye moduli ya msingi ya kituo cha anga ya juu cha Tianhe ndani ya chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-14 Tarehe 5, Juni mwaka huu kwa ajili ya kukaa kwa miezi sita.

Ujumbe huo wa wanaanga umetumia zaidi ya siku 170 katika obiti. Hii ni mara ya pili kwa Chen kuelekea anga ya juu, kufuatia misheni yake ya kwanza ya siku 33 ya chombo cha Shenzhou-11 kwenye kituo cha anga ya juu cha Tiangong-2, ambacho ni kituo kitangulizi cha anga ya juu, Mwaka 2016 akiwa na mwanaanga Jing Haipeng.

"Chen ni mtu anayependa ukamilifu. Haachi kamwe matatizo bila kutatuliwa," Jing amesema. Baada ya safari yake ya kwanza ya anga ya juu, Chen alitunukiwa medali ya ngazi ya tatu na hadhi ya heshima ya "mwanaanga shujaa."

Chen alizaliwa Mwaka 1978 katika Mkoa wa Henan, katikati mwa China. Aliajiriwa katika timu ya wanaanga wa China Mei 2010.

Akiwa ameteuliwa kama kamanda wa misheni, Chen amewaongoza wanaanga wa chombo cha Shenzhou-14 kukamilisha kazi nyingi katika muda wa miezi mitano iliyopita, ikiwa ni pamoja na safari tatu za anga ya juu, mfululizo wa majaribio ya kisayansi, mihadhara ya sayansi ya moja kwa moja, na shughuli kadhaa wa kadhaa.

Picha hii ya skrini iliyopigwa katika Kituo cha Udhibiti wa Anga ya Juu cha Beijing Novemba 17, 2022 ikionyesha mwanaanga wa China kwenye chombo cha Shenzhou-14 Chen Dong akiwa ametoka kwenye moduli ya maabara ya Wentian ya kituo cha anga ya juu cha China. Wanaanga wa Shenzhou-14 walio kwenye kituo cha anga ya juu cha Tiangong cha China kinachozunguka wanaendesha shughuli zao za ziada kwa mara ya tatu. (Picha na Sun Fengxiao/Xinhua)

Katika misheni hiyo, wanaanga hao watatu katika obiti walisimamia kuwasili kwa moduli mbili za maabara za kituo, Wentian na Mengtian, na kushuhudia vyombo viwili vya anga ya juu, Tianzhou-4 na Tianzhou-5. Pia watashuhudia wakati wa kihistoria ambapo kituo cha anga ya juu cha China kitakamilika kikamilifu mwishoni mwa mwaka huu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha