Maktaba za kidijitali zaangazia dunia ya rohoni mwa watu wenye matatizo ya kuona nchini China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 24, 2022

Msomaji mwenye matatizo ya kuona (wa pili kulia) akijaribu mwongozo wa roboti kwenye maktaba ya kidijitali ya Jinan, Mkoa wa Shandong, China, Oktoba 14, 2022. (Xinhua/Yuan Min)

JINAN - Zhang Xuejing hivi majuzi alifurahia filamu nzuri pamoja na watu wengine wanane wenye matatizo ya kuona kwenye maktaba katika Mkoa wa Shandong, Mashariki mwa China.

Lilikuwa toleo lisilo na kizuizi la filamu ya The Magical Brush, ambayo ni maarufu nchini China. Sauti ya maelezo ya filamu hiyo iliongezwa ili kusaidia hadhira maalum kuelewa hadithi.

"Maelezo yalikuwa wazi sana kiasi kwamba nilihisi nilikuwa karibu na mhusika mkuu jasiri na mwerevu Ma Liang," Zhang anasema. "Kila wakati ninapokuwa kwenye ukumbi wa sinema ninahisi kuburudishwa na kufurahishwa."

Filamu zisizo na vizuizi ni moja ya huduma za kidijitali ambazo Maktaba ya Shandong imezindua ili kuimarisha maisha ya kitamaduni ya walemavu wa macho. Mapema Mwaka 2013, maktaba ilianzisha mradi wa maktaba ya kidijitali kwa ajili ya watu wa kundi hilo maalumu, ikibadilisha vitabu vya nakala ngumu kuwa nyenzo za sauti zinazoweza kufikiwa mtandaoni. Hadi sasa, jumla ya hifadhi ya data ya rasilimali za kidijitali imefikia terabaiti 15 na zaidi ya watembeleaji milioni 3.

Kupitia uratibu na maktaba 17 za umma kote Shandong, maktaba ya mkoa imesambaza seti 15,000 za vichezeshi mahiri vya vitabu vya sauti bila malipo.

"Kusoma siyo tu kupata ujuzi , bali pia ni kurutubisha roho," anasema Zhou Yushan, Naibu Mkurugenzi wa Maktaba ya Shandong, huku akiongeza kuwa maktaba za kidijitali zimekuwa kimbilio la kiroho kwa wasomaji wenye matatizo ya kuona.

Wakati Zhang alipopoteza uwezo wake wa kuona miaka miwili iliyopita kutokana na ugonjwa na kulazimika kuacha kazi yake, alijihisi kuwa chini kwenye madampo. Kwa bahati nzuri, kwenye maktaba ya kidijitali, alijifunza hati nundu na kupata marafiki walio katika hali sawa na yake. Walimweleza kuhusu fursa nyingi za ajira kwa watu wenye matatizo ya kuona, kama vile kazi za kuboresha sauti za kinanda, ushauri wa kisaikolojia na uimbaji, jambo ambalo liliongeza matumaini ya Zhang ya maisha mapya.

Sasa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 42 ni mtangazaji wa maudhui kwenye mtandao wa podcast akiwa na wafuatiliaji wengi. Yeye husoma na kushiriki mashairi na makala nzuri, na amebuni kozi za kisaikolojia ili kutoa msaada wa kiroho kwa hadhira yake.

China imekuwa ikitangaza huduma za kitamaduni kila mara kwa makundi ya watu wenye ulemavu. Mwaka 2017, Baraza la Serikali la China lilitoa mipango ya kuendeleza ufikiaji sawa wa huduma za kimsingi za umma, ikielekeza serikali za mitaa kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wana ufikiaji usio na kizuizi kwa bidhaa na huduma za kitamaduni na watu kama hao wanaweza kufurahia televisheni, filamu, michezo na kazi nyingine za utamaduni.

Hadi sasa, Shandong imejenga vyumba 83 vya kusoma kidijitali nje ya mtandao katika shule maalum, maktaba za umma na vituo vya huduma kwa walemavu, na maktaba 181 katika mkoa huo zimeweka maeneo ya kusoma kwa watu wenye ulemavu wa macho.

"Ninaweza kuhisi kuwa jamii sasa inathamini na inawajali zaidi wasioona, na tuna fursa zaidi za maendeleo," Zhang amesema, huku akiongeza kuwa anatumai kubadilishana uzoefu wake na watu wenye mahitaji na kuhimiza watu wengi zaidi wenye matatizo ya kuona kujumuika katika jamii.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha