Rais Xi na mwenzake wa DRC Tshisekedi wapongezana kwa kuadhimisha miaka 50 tangu uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na DRC uwe wa kawaida

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2022

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi Alhamisi walitumiana salamu za pongezi kwa kuadhimisha miaka 50 tangu uhusiano wa kidiplomasia urudi katika hali ya kawaida kati ya nchi hizo mbili.

Rais Xi amesema katika ujumbe wake kwamba katika kipindi cha nusu karne iliyopita, uhusiano kati ya China na DRC umeendelea kwa njia nzuri na thabiti, na urafiki wa jadi umezidi kuimarishwa.

Ameongeza kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizo mbili zimeanzisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote na kupata matokeo yenye matunda katika ushirikiano wa kivitendo, ambao umeleta manufaa zaidi kwa watu wa pande mbili.

Xi amesema, anatilia maanani sana maendeleo ya uhusiano wa pande hizo mbili, na yuko tayari kushirikiana na Rais Tshisekedi kuchukua maadhimisho ya miaka 50 kama fursa ya kuzidisha kuaminiana kisiasa, kuimarisha ushirikiano wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na kufungua kwa pamoja matarajio mapya kwa uhusiano kati ya China na DRC.

Kwa upande wake, Tshisekedi kwa mara nyingine tena ametoa pongezi za dhati kwa Rais Xi kwa kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, akisema kuwa katika kipindi cha nusu karne iliyopita, uhusiano wa nchi hizo mbili umepata maendeleo endelevu na mazuri.

Ameeleza kuwa yuko tayari kuimarisha urafiki wa jadi kati ya nchi hizo mbili na kusukuma mafanikio mapya katika ushirikiano wa kimkakati kati ya DRC na China kwa manufaa ya watu wao.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha