Tanzania yatangaza mgao wa umeme kutokana na ukame wa muda mrefu

(CRI Online) Novemba 25, 2022

Shirika la Umeme nchini Tanzania (TANESCO) limetangaza rasmi mgao wa umeme kote nchini humo kutokana na ukame wa muda mrefu ambao umesababisha kupungua kwa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.

Taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Maharage Chande imesema, uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo mbalimbali umepungua kwa kati ya MW 300 hadi MW 350 kwa siku, na kuongeza kuwa kati ya vyanzo hivyo, uzalishaji wa umeme kwa maji unachangia MW 181 kwa siku.

Taarifa hiyo imesema TANESCO imekuwa ikitekeleza mipango ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu ambayo inalenga kupunguza upungufu wa umeme nchini humo kwa kuwa mgao wa sasa wa kila siku ni wa saa nane hadi 12.

Taarifa hiyo imetaja mipango hiyo kuwa ni kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme, na ujenzi wa Mradi wa Uzalishaji Umeme kwa Maji wa Bwawa la Julius Nyerere.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha