Mchakato wa kijadi wa uandaaji chai wa China waingia kwenye orodha ya urithi wa kitamaduni wa UNESCO

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 30, 2022

Kipengele cha "Mbinu za kijadi za usindikaji wa chai na desturi zinazohusiana nazo za kijamii nchini China" kikichunguzwa kwenye Mkutano wa 17 wa Kamati ya Kiserikali ya Kulinda Urithi wa Utamaduni Usioshikika ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) huko Rabat, Morocco, Novemba 29, 2022. Mchakato wa Uandaaji wa chai wa jadi wa China Jumanne umeingizwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioshikika na UNESCO katika mji mkuu wa Morocco wa Rabat. (Xinhua/Xu Supei)

RABAT - Mchakato wa kijadi wa uandaaji chai wa China Jumanne umeingizwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioshikika na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Kipengele cha "Mbinu za kijadi za usindikaji wa chai na desturi zinazohusiana nazo za kijamii nchini China" kilifaulu mtihani huo kwenye Mkutano wa 17 wa Kamati ya Kiserikali ya Kulinda Urithi wa Utamaduni Usioshikika ya UNESCO huko Rabat, Morocco.

China sasa ina vitu 43 kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioshikika, ikiendelea kuwa nchi yenye vitu vingi vilivyoorodheshwa zaidi duniani.

Wang Yongjian, mkuu wa ujumbe wa China kwenye mkutano wa UNESCO, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kuwa maamuzi hayo yatafanya urithi huo wa kitamaduni uonekane zaidi kwa umma na kusaidia kukuza heshima ya utofauti wa kitamaduni na ubunifu wa binadamu.

"Tutaomba na kutangaza zaidi miradi ya urithi wa utamaduni usioshikika na umaalumu wa China na kuonyesha roho na hekima ya China, ili kuhimiza zaidi utamaduni wa China kwenda kimataifa," ameongeza.

Mbinu za kitamaduni za usindikaji wa chai na mazoea ya kijamii yanayohusiana nazo nchini China zinajumuisha maarifa, ujuzi, na mazoea kuhusu usimamizi wa mashamba ya chai, kuchuma majani ya chai, usindikaji kwa mikono, kunywa, na kushiriki chai.

Tangu zama za kale, Wachina wamekuwa wakipanda, kuchuma, kuandaa na kunywa chai. Wazalishaji wa chai wameanzisha aina sita za chai: kijani, njano, nyekundu, nyeupe, oolong na chai nyeusi. Pamoja na chai iliyochakatwa, kama vile chai yenye harufu ya maua, kuna zaidi ya bidhaa 2,000 za chai nchini China.

Chai hupatikana kila mahali katika maisha ya kila siku ya Wachina, kwani chai ya maji au iliyochemshwa hutolewa katika familia, mahali pa kazi, nyumba za chai, mikahawa na mahekalu, kwa kutaja chache. Pia hutumika kama sehemu muhimu ya kujenga ujamaa miongoni mwa watu na sherehe kama vile harusi na dhabihu, UNESCO imeongeza.

Mkutano huo wa UNESCO, ulioanza Novemba 28 na umepangwa kuendelea hadi Desemba 3, unachunguza vipengele 46 vilivyowasilishwa na nchi mbalimbali duniani ili kuorodheshwa kwenye Orodha Wakilishi ya Urithi wa Utamaduni wa Binadamu Usioshikika, vipengele vinne vya Orodha ya Urithi Usioshikika Unaohitaji Ulinzi wa Haraka, vitu vitano kwa Rejista ya Mazoea Bora ya Ulinzi, na ombi moja la Usaidizi wa Kimataifa.

Picha hii iliyopigwa Tarehe 29 Novemba 2022 ikionyesha shughuli ya Mkutano wa 17 wa Kamati ya Kiserikali ya Kulinda Urithi wa Utamaduni Usioshikika ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) huko Rabat, Morocco, Novemba 29, 2022. (Xinhua/Xu Supei)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha