

Lugha Nyingine
China yasaidia mapambano dhidi ya umaskini barani Afrika kupitia ushirikiano wa kilimo
BUJUMBURA - Kwenye mchana wa jua kali, Charles Ngendakumana, mkulima katika Mkoa wa Bubanza Kaskazini-Magharibi mwa Burundi, alikuwa na shughuli nyingi za kuongeza nyasi kwenye zizi la ng'ombe, nyuma ya nyumba yake mpya ya kijijini iliyojengwa hivi karibuni, aina ya bungalow yenye ghorofa moja na kuta za chokaa zilizopakwa rangi mpya.
Karibu naye, kuku wapatao kumi walikuwa wakikimbia huku na huko. Akiwanyooshea kidole, alisema kuku hao wamepewa kwa familia yake na wataalamu wa kilimo kutoka China. "Pia walitoa mbegu nzuri za mpunga na mbolea na kunifundisha mbinu za kupanda ili niwe na chakula cha kutosha kulisha watoto wangu", baba huyo wa watoto sita mwenye umri wa miaka 43 anasema.
Miaka minne iliyopita, Ngendakumana alianza kupanda mpunga chotara ulioletwa kutoka China chini ya uongozi wa wataalamu wa kilimo wa China. Tangu wakati huo, shamba lake pia limeongezeka kutoka nusu hekta hadi hekta tano huko Ninga, kijiji katika Wilaya ya Gihanga.
"Siku zijazo, nataka kununua ardhi zaidi, ng'ombe zaidi, pamoja na pampu mpya kadhaa za kusukuma maji msimu wa kiangazi utakapofika," Ngendakumana amesema katika mahojiano ya hivi karibuni na Shirika la Habari la China, Xinhua, huku akisisitiza kwamba hii ilikuwa "haiwezekani" katika siku chache kabla ya kuwasili kwa timu za wataalam wa China ambapo hakuweza hata kupata chakula cha kutosha.
Ikijulikana kama "moyo wa Afrika", nchi ya Burundi iliyoko Afrika Mashariki ina hali ya hewa ya kitropiki yenye mvua nyingi. Hali yake ya asili ni nzuri kwa uzalishaji wa mpunga, lakini kuzalisha mavuno kidogo ya mpunga wa kienyeji kuliwafanya Warundi kuteseka kwa muda mrefu kutokana na uhaba wa chakula.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, China imekuwa ikitekeleza mipango ya ushirikiano wa kitaalamu nchini Burundi kuanzia Agosti, 2009, na kutuma jumla ya wataalam 45 katika nchi hiyo ya Afrika katika makundi matano kusaidia kuendeleza kilimo.
Wataalamu hao wa China kwa sasa wanapanda mpunga chotara katika vijiji 22 nchini humo katika juhudi za kusaidia kutimiza kauli mbiu ya Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi -- "Kila mdomo una chakula na kila mfuko una pesa."
Wataalamu hao wametembelea mashamba katika majimbo yote 14 yanayolima mpunga nchini humo kufanya utafiti na majaribio, na kufanikiwa kuchagua na kutambulisha aina nane za mbegu za mpunga zinazoendana na hali ya Burundi.
Ushirikiano wa kilimo kwa lengo la kupunguza umaskini vijijini barani Afrika umekuwa eneo muhimu la ushirikiano kati ya China na Afrika katika miaka ya hivi karibuni. Wakati wa Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwaka mmoja uliopita nchini Senegal, China ilitangaza kuwa itatekeleza miradi ya kupunguza umaskini na kuendeleza kilimo na Afrika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Kama sehemu ya mpango huo, China itatuma wataalam 500 wa kilimo barani Afrika, kuanzisha vituo kadhaa vya pamoja vya kubadilishana teknolojia za kisasa za kilimo, mifano halisi na mafunzo nchini China, na kuhimiza taasisi na makampuni ya China kujenga barani Afrika vijiji vya vielelezo vinavyosaidia maendeleo ya kilimo na kupunguza umaskini.
Miradi kadhaa inatekelezwa pia katika kijiji cha Matangi Tisa katika Kaunti ya Nakuru nchini Kenya katika na Kijiji cha Kielelezo cha Maendeleo ya Kilimo na Kupunguza Umaskini kati ya China na Afrika cha Shimwengwe katika Mkoa wa Lusaka nchini Zambia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma