Ushirikiano kati ya China na Afrika wasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 21, 2022

Picha ikionesha Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa nishati ya Jua cha Sakai kilichofadhiliwa na China huko Bimbo, Jamhuri ya Afrika ya Kati. (Picha/Xinhua)

Kenya ni moja ya nchi za pembe ya Afrika zinazokumbwa zaidi na ukame mbaya uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ambao haujawahi kushuhudiwa katika miaka 40 iliyopita. Katika pembe nzima ya Afrika, hadi mwisho wa mwaka huu kutakuwa na watu zaidi ya milioni 36 wanaoathiriwa na ukame wa muda mrefu, wakiwemo Wakenya milioni 4.5, ikiwa ni matokeo ya upungufu wa mvua za masika kwa misimu mitano mfululizo, ilisema Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa mwezi uliopita.

“Mpito wa nishati umekuwa wajibu wetu sote duniani, hasa kwa upande wa athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Rais Nana Addo Dankwa Akufo-Addo wa Ghana kwenye mkutano wa COP27, akiongeza kuwa, Ghana inajikita kwenye kuongeza uwiano wa nishati mbadala katika muundo wa umeme wake, na kuchunguza uwezo wa nishati ya hydrogen na nishati nyingine safi.

Huku nchi za Afrika zinajikita kwenye kuendeleza nishati mbadala ili kupunguza utoaji wa hewa chafu, wataalamu wanakadiria kuwa ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta hiyo utaongezeka.

“Nishati safi ni sehemu muhimu ya ushirikiano kati ya China na Afrika,” anasema msomi wa masomo ya uhusiano wa kimataifa wa Kenya Cavince Adhere, akiongeza kuwa China imeonyesha nia yake ya kushirikiana na nchi za Afrika katika mpito wa nishati mbadala.

Chini ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, ambalo ni baraza muhimu la ushirikiano wa pande mbili, China imetekeleza miradi 100 hivi ya nishati safi na maendeleo ya kijani katika miaka iliyopita.

Miradi hiyo ni pamoja na kiwanda cha uzalishaji wa umeme kwa nishati ya jua cha Garissa, ambacho kinazalisha umeme wa kukidhi mahitaji ya watu zaidi ya 380,000 kila mwaka tangu kilipozinduliwa Mwaka 2019.

Licha ya hayo, Kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya maji cha Bonde Kafue nchini Zambia, Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa nishati ya Upepo wa Aysha nchini Ethiopia, na Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa nishati ya Jua cha Sakai nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati vyote vinatoa nishati mbadala kwa wakazi huko.

Karibu umbali wa kilomita 160 kutoka Kusini mwa Nairobi, Bwawa la Thwake, bwawa kubwa zaidi la matumizi mbalimbali linalojengwa nchini Kenya, ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80.

Bwawa hilo linalojengwa na Shirika la Gezhouba la China, litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo milioni 688. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha