China yajenga ukanda mkubwa zaidi wa nishati safi duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 21, 2022

Picha iliyopigwa Tarehe 24 Novemba, 2022 ikionyesha kituo cha kufua umeme cha Baihetan, ambacho kinazunguka mikoa ya Yunnan na Sichuan Kusini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Xu Bingjie)

CHENGDU - Kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya maji cha Baihetan, ambacho ni cha pili kwa ukubwa duniani kwa uwezo wake wa kuzalisha umeme, kimeanza kufanya kazi kikamilifu Jumanne wiki hii katika sehemu ya juu ya Mto Changjiang Kusini-Magharibi mwa China, kwa mujibu wa Shirika la China Magenge Matatu.

Kuanza kwake kufanya kazi kunaashiria kukamilika kwa ukanda mkubwa zaidi wa nishati safi duniani, ambapo vituo sita vya kuzalisha umeme kwa nguvu za maji kwenye Mto Changjiang vinafanya kazi ya kusambaza umeme kutoka eneo la Magharibi lenye rasilimali nyingi hadi mikoa inayotumia nishati nyingi ya Mashariki mwa China.

Kuanza kufanya kazi kikamilifu kwa Kituo cha Baihetan kunakuja baada ya mashine ya mwisho kati ya 16 ya kuzalisha umeme kwa nishati ya maji kukamilisha oparesheni ya majaribio ya saa 72 Jumanne asubuhi. Ikiwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya kilowati milioni 16 za umeme, Bwawa la Baihetan ni la pili baada ya mradi wa Bwawa la Magenge Matatu katika mkoa wa kati wa China wa Hubei.

Picha hii iliyopigwa Tarehe 25 Novemba 2022 ikionyesha kituo cha kuzalisha umeme cha Wudongde kwenye mpaka wa mikoa ya Sichuan na Yunnan, Kusini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Xu Bingjie)

"Baihetan inaashiria mafanikio makubwa katika utengenezaji wa vifaa vya teknolojia ya hali ya juu nchini China, kwani ina mashine 16 za kuzalisha umeme kwa nishati ya maji zilizoundwa nchini China, kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha umeme wenye nguvu ya kilowati milioni 1, kiasi ambacho ni kikubwa zaidi kwa mashine moja duniani," amesema Lei Mingshan, Mwenyekiti wa Shirika la China la Magenge Matatu.

Vituo sita vya kuzalisha umeme kwa nishati ya maji kwenye Mto Changjiang , vyote vinavyoendeshwa na shirika hilo, vinatarajiwa kuzalisha umeme wa kiasi cha kilowati bilioni 300 kila mwaka, na kupunguza matumizi ya makaa ya mawe kwa tani milioni 90 na utoaji wa kaboni kwa tani milioni 248.

Picha hii iliyopigwa Tarehe 24 Novemba 2022 ikionyesha mashine za kuzalisha umeme kwa nishati ya maji ya kituo cha kuzalisha umeme cha Baihetan, ambacho kinatapakaa katika mikoa ya Yunnan na Sichuan, Kusini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Xu Bingjie)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha