

Lugha Nyingine
China yapunguza hatua za kudhibiti UVIKO-19 kutoka Ugonjwa Hatari wa Kuambukiza Daraja A hadi Daraja B na kuondoa hatua za karantini
BEIJING - China itaanza kudhibiti UVIKO-19 kwa kuchukua hatua zinazoendana na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ya Hatari Daraja B, badala ya magonjwa ya kuambukiza ya Hatari Daraja A, katika mabadiliko makubwa ya sera zake za kukabiliana na janga hilo.
China imebadilisha jina na hadhi ya UVIKO-19 kutoka "pneumonia mpya ya virusi vya Korona" hadi "maambukizi mapya ya virusi vya Korona," imesema taarifa iliyotolewa na Kamati ya Taifa ya Afya ya China siku ya Jumatatu.
Kuanzia Januari 8 mwakani, China itashusha nafasi ya udhibiti wa ugonjwa huo kutoka Daraja A hadi B kwa mujibu wa sheria ya nchi hiyo ya kuzuia na kutibu magonjwa ya kuambukiza, na itauondoa ugonjwa huo katika orodha ya magonjwa ya kuambukiza yanayohitaji hatua za karantini kwa mujibu wa Sheria ya Afya na Karantini ya Jamhuri ya Watu wa China, imeongeza taarifa hiyo.
Hivi sasa, UVIKO-19 umeainishwa kama ugonjwa wa kuambukiza wa Daraja B lakini unashughulikiwa kwa hatua za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa kuambukiza wa Hatari Daraja A nchini China.
Masharti ya kimsingi yamewekwa ili kuunga mkono marekebisho hayo, imesema taarifa iliyotolewa na kikundi kazi cha kuzuia na kudhibiti UVIKO-19 cha Baraza la Serikali la China siku hiyo hiyo, huku ikitoa mfano wa mabadiliko ya hivi karibuni ya virusi, maendeleo ya kudhibiti janga hilo na mwitikio wa nchi ya China katika kudhibiti janga.
Serikali Kuu na za mitaa nchini China zitaondoa hatua za kuwaweka watu walioambukizwa virusi vya Korona karantini na kuacha kutambua watu waliokutana kwa ukaribu na walioambukizwa au kuyatenga maeneo yenye hatari kubwa na hatari ndogo ya maambukizi, imesema taarifa hiyo.
Wagonjwa wa UVIKO-19 watapata matibabu yaliyoainishwa na marekebisho ya wakati yatafanywa kwa sera za matibabu. China pia itarekebisha sera zake za kupima pamoja na mfululizo na maudhui ya utoaji wa taarifa za janga.
Aidha, hatua za kudhibiti magonjwa zinazolenga wasafiri wanaoingia nchini China pamoja na mizigo kutoka nje zitaondolewa, imesema taarifa hiyo.
Kufuatia marekebisho hayo, juhudi za China za kuzuia na kudhibiti UVIKO-19 zitatilia maanani kulinda afya na kuzuia maambukizi makali.
Hatua zitachukuliwa ili kulinda maisha na afya ya watu kwa kiwango kikubwa na kupunguza athari za janga hili katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma