Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping wa China atoa salamu za mwaka mpya wa 2023
(Picha inatoka CRI.)
Katika mkesha wa mwaka mpya, rais Xi Jinping wa China ametoa salamu za mwaka mpya wa 2023 kupitia Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG) na mtandao wa Internet. Ifuatayo ni salamu hizo:
Makomredi, marafiki, mabibi na mabwana:
Hamjambo!
Wakati mwaka 2023 umewadia, mimi nikiwa hapa Beijing napenda kuwapa salamu za mwaka mpya.
Mwaka 2022, tulifanya kwa mafanikio Mkutano mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China, ambapo tulitunga mpango kabambe wa kujenga nchi ya kisasa ya kijamaa na kufanikisha ustawishaji wa taifa la China katika mchakato wa kujenga nchi ya kisasa ya mtindo wa Kichina, ndio maana tulitoa wito wa kuanza safari mpya.
China imeendelea kuwa nchi ya pili duniani kwa ukubwa wa uchumi, uchumi wake uliendelea kukua kwa hatua madhubuti, na pato la taifa kwa mwaka 2022 linatarajiwa kuzidi Renminbi Yuan trilioni 120, sawa na dola trilioni 17.15 za kimarekani. Wakati msukosuko wa chakula ulipoisumbua dunia nzima, China ilipata mavuno makubwa ya nafaka kwa miaka 19 mfululizo, mafanikio ambayo yamewahakikisha wananchi wa China chakula cha kutosha. Tuliimarisha mafanikio tuliyopata katika kazi ya kuondokana na umaskini, na kusukuma mbele shughuli za kuendeleza sehemu za vijijini. Vile vile tulichukua hatua mbalimbali za kuondoa shida za makampuni na viwanda, kama vile kupunguza mzigo wa kodi na ushuru, na kufanya chini juu kutatua matatizo yanayowasumbua wananchi wetu.
Baada ya kulipuka kwa maambukizi ya COVID-19, siku zote tulishikilia moyo wa kutoa kipaumbele kwa umma na maisha, na hatua zetu za kukinga na kuzuia maambukizi zilirekebishwa kwa kufuata sayansi na mabadiliko ya hali halisi, ndio maana usalama wa maisha na afya ya wananchi wetu vimelindwa kwa kiwango cha juu. Watu wa China, hususan madaktari na wauguzi, pamoja na makada kwenye ngazi ya mashina, wamechapa kazi kwa ushujaa bila kujali ugumu na shida. Kutokana na jitihada kubwa na kazi ngumu, tumeshinda shida na changamoto kubwa ambazo hazijawahi kutokea, kila mwananchi amefanya bidii. Hivi sasa kazi ya kukinga na kuzuia maambukizi ya COVID-19 imeingia katika kipindi kipya, ambacho bado ni kipindi kigumu, sisi sote tunajitahidi na matumaini yameonekana. Tufanye jitihada kubwa zaidi, tuvumilie na kushikamana hadi tutakapopata ushindi wa mwisho.
Mwaka 2022, komredi Jiang Zemin alifariki dunia. Tunakumbuka mchango wake mkubwa na moyo wake mwema, na kuthamini mali aliyoturithisha ya kiroho yenye thamani kubwa. Tunapaswa kurithi nia yake, na kuendelea kusukuma mbele shughuli za ujamaa wenye umaalum wa China katika zama mpya.
Historia ni kama mto wenye mawimbi makubwa, na watu wameijenga China ya leo kizazi baada ya kizazi.
China ya leo ni China inayotimiza ndoto moja baada ya nyingine. Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi, na Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Majira ya Baridi ilifanyika kwa mafanikio mjini Beijing, na wachezaji walishindana viwanjani na kupata matokeo mazuri. Vyombo vya safari za Anga ya Juu vya Shenzhou No. 13, No. 14 na No. 15 vilirushwa kwa mafanikio kwa nyakati tofauti, na ujenzi wa Kituo cha Anga ya Juu ya China ulikamilika, ambapo sasa “Nyumba yetu Angani” inasafiri kwenye anga ya juu. Huu ni mwaka wa 95 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Ukombozi wa umma la China, na wanajeshi wa China wanasonga mbele katika mchakato wa kujiimarisha. Manowari ya tatu ya kubeba ndege za kivita ya Fujian ilizinduliwa, ndege kubwa ya kwanza ya abiria aina ya C919 ilikabidhiwa kwa shirika la ndege, Kituo cha Umeme kwa Nishati ya Maji ya Baihetan kilianza kuzalisha umeme… Mafanikio hayo yanatokana na juhudi za watu wengi. Mshikamano ndio nguvu ya China.
China ya leo ni China yenye uhai mkubwa. Maeneo mbalimbali ya biashara huria ukiwemo mkoa wa biashara huria wa Hainan yanastawi. Sehemu zilizoko karibu na bahari zinafanya uvumbuzi kwa hatua madhubuti. Sehemu za katikati na magharibi zinaharakisha maendeleo. Sehemu za kaskazini mashariki ziko tayari kustawi tena. Na Sehemu za mipakani zinajiendeleza na kuboresha maisha ya watu. Hali ya kimsingi ya uchumi wa China ya kuwa na uvumilivu, uwezo na uhai mkubwa na mwelekeo wa kuwa mzuri zaidi kwa muda mrefu haijabadilika. Tukiwa na imani thabiti na kuuendeleza uchumi kwa utulivu, hakika tutatimiza lengo tuliloweka. Mwaka huu nilikwenda Hong Kong, nilifurahia kuona mkoa huo umerejesha utulivu na ustawi. Tukitekeleza vizuri mfumo wa Nchi Moja, Mifumo Miwili kwa nia thabiti, Hong Kong na Macao hakika zitadumisha ustawi na utulivu wa muda mrefu.
China ya leo ni China inayorithi moyo wa kitaifa. Katika mwaka wa 2022, tulikumbana na majanga mbalimbali ya asili ikiwa ni pamoja na matetemeko ya ardhi, mafuriko, ukame, na moto wa misituni, na pia kushuhudia ajali kubwa za uzalishaji. Kati ya matukio hayo ya kutia wasiwasi na kuhuzunisha, zimetokea hadithi nyingi za kugusa mioyo ya watu walioshikamana katika wakati mgumu au hata kujitoa mhanga ili kusaidia wengine walio katika dhiki. Matendo hayo ya kishujaa yatawekwa kwenye kumbukumbu zetu milele. Kila ifikapo mwisho wa mwaka, huwa tunakumbuka moyo mtukufu wa taifa letu uliorithiwa kwa maelfu ya miaka, ambao unatupa imani zaidi tunapoendelea kusonga mbele.
China ya leo ni China yenye uhusiano wa karibu na dunia. Katika mwaka uliopita, niliwakaribisha mjini Beijing marafiki wengi, wakiwa wa zamani na wapya, na pia nilisafiri nje ya nchi ili kuwasilisha mapendekezo ya China kwa dunia. Mabadiliko ambayo hayajaonekana katika karne moja iliyopita yanaendelea kwa kasi kubwa, na dunia bado sio mahali tulivu. Tunathamini amani na maendeleo, na tunathamini marafiki na wenzi kama tulivyofanya siku zote. Tunasimama kidete katika upande sahihi wa historia na upande wa ustaarabu na maendeleo ya binadamu. Tunafanya kazi kwa bidii kuchangia busara na mipango ya China kwa ajili ya amani na maendeleo ya binadamu wote.
Baada ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), mimi na wenzangu tulitembelea Yan'an, ambapo tulirudia kipindi cha kutia moyo ambapo uongozi mkuu wa Chama ulishinda matatizo ya ajabu katika miaka ya 1930 na 1940, na kutafakari kuhusu nguvu ya kiroho ya kizazi kikongwe cha wanachama wa CPC. Mara nyingi mimi husema, "Kama vile kung'arisha hufanya jade kuwa nzuri zaidi, shida humfanya mtu awe na nguvu zaidi." Katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, CPC imestahimili upepo na mvua, na kusonga mbele dhidi ya changamoto mbalimbali. Hii ni safari ngumu lakini kubwa zaidi. Leo, lazima tusonge mbele kwa ujasiri ili kuifanya China ya kesho kuwa mahali pazuri zaidi.
China ya kesho itafanya miujiza kupitia kufanya kazi kwa bidii. Hapa nataka kumnukuu Su Shi, mshairi mashuhuri wa China, “ukitatua tatizo zaidi, utafika mbali zaidi." Maneno hayo yanahimiza watu “kujitahidi kwenye sehemu zenye changamoto zaidi na kutafuta malengo makubwa zaidi”. Tukiendelea kusafiri, tutafika bila ya kujali umbali, tukiendelea kujitahidi, tufafanikisha kazi yoyote. Kama tuna azma ya kuhamisha milima na uvumilivu wa kusonga mbele, ilimradi tu tunaweka miguu yetu chini na kusonga mbele na safari yetu kwa kutafuta maendeleo thabiti, tutageuza malengo yetu makuu kuwa hali halisi.
China ya kesho inategemea mshikamano. China ni nchi kubwa, ni jambo la kawaida kuwa watu mbalimbali kuwa na matakwa tofauti na maoni tofauti juu ya jambo moja, na maafikiano yanapaswa kufikiwa kupitia mawasiliano na majadiliano. Wachina zaidi ya bilioni 1.4 wakiwa na nia moja na kufanya kazi kwa ushirikiano kwa ajili ya lengo moja, hakuna jambo lisiloweza kufanikiwa au vikwazo visivyoweza kuondolewa. Watu wa pande mbili za mlango bahari wa Taiwan ni ndugu wa familia moja. Natumai kwa moyo wa dhati kuwa ndugu wa pande hizo zote mbili watasonga mbele kwa lengo la pamoja ili kujenga ustawi wa muda mrefu wa taifa la China.
China ya kesho inategemea vijana. Vijana wakiwa hodari, nchi itastawi. Maendeleo ya China yanategemea ujasiri na uwajibikaji wa vijana. Ujana umejaa uchamgamfu, na vijana huleta matumaini. Vijana wanatakiwa kuwa na uzalendo, kufanya kazi kwa bidii bila ya kutumia ovyo ujana wao na fursa za zama mpya.
Katika wakati huu, watu wengi bado wanafanya kazi kwa bidii, poleni sana! Kengele ya mwaka mpya inakaribia kulia, tukaribishe kwa pamoja miale ya kwanza ya jua ya mwaka 2023 tukiwa na matumaini kwa mustakabali mzuri.
Natakia nchi yetu ustawi na amani, na watu kuwa na usalama! Naitakia dunia nzima amani, furaha na utulivu! Nawatakieni ninyi nyote heri ya mwaka mpya na ndoto zenu zote zitimizwe!
Asanteni!
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma