China yatoa mkopo nafuu kwa mradi wa mkongo wa taifa wa intaneti wa Angola

(CRI Online) Januari 13, 2023

China itatoa uungaji mkono wa kifedha kwa mradi wa mkongo wa taifa wa intaneti nchini Angola chini ya makubaliano ya mkopo wenye masharti nafuu yaliyosainiwa jana.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Benki ya Exim ya China itatoa mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 249 kwa ajili ya ujenzi wa kebo ya mkongo wenye urefu wa kilomita 2,000 nchini Angola, pamoja na nyingine ya chini ya maji inayounganisha eneo la Cabinda, na kuboresha mkongo wa mawasiliano wa nchi hiyo.

Makubaliano hayo yalisainiwa na balozi wa China nchini Angola, Gong Tao na waziri wa fedha wa Angola Vera Daves de Sousa mjini Luanda.

Mradi huo utahakikisha ufikiaji wa huduma za mtandao kwa kasi kwenye maeneo ya mbali nchini Angola, kupunguza gharama za huduma na kupiga jeki uchumi wa kidijitali wa nchi hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha